Mchezaji bosi! Ng’olo Kante anunua klabu ya soka Ubelgiji baada ya kuondoka Chelsea

Kante ndiye mmiliki mpya wa klabu ya soka ya Ubelgiji, Royal Excelsior Virton.

Muhtasari

•Kante atachukua usukani wa klabu hiyo ambayo ni inashiriki katika ligi ya daraja la tatu ya Ubelgiji kuanzia Julai 1 baada ya kukamilisha ununuzi kutoka kwa Flavio Becca.

•Kante na washirika wake wamekubaliana masharti ya kuchukua udhibiti wa klabu hiyo ya Ubelgiji, ambayo ilishushwa daraja hadi ngazi ya tatu ya soka ya Ubelgiji.

N'golo Kante
Image: HISANI

Kiungo wa zamani wa Chelsea, N’golo Kante ndiye mmiliki mpya wa klabu ya soka ya Ubelgiji, Royal Excelsior Virton.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 32 atachukua usukani wa klabu hiyo ambayo ni inashiriki katika ligi ya daraja la tatu ya Ubelgiji kuanzia Julai 1 baada ya kukamilisha ununuzi kutoka kwa Flavio Becca.

"Flavio ni wazi ana furaha kubwa kuweza kukabidhi mikoba ya klabu kwa N'Golo Kante," Royal Excelsior Virton ilisema katika taarifa.

Kante na washirika wake wamekubaliana masharti ya kuchukua udhibiti wa klabu hiyo ya Ubelgiji, ambayo ilishushwa daraja hadi ngazi ya tatu ya soka ya Ubelgiji.

Klabu hiyo ilimaliza katika nafasi ya 12 na mkiani mwa Ligi ya Challenger Pro, ikikosa kunusurika kwa pointi moja tu, na Kante ataongoza kazi ya kuijenga upya.

"Kwa kuendeshwa na mapenzi yake kwa soka, nia ya N'Golo Kante ni kuendeleza muundo wa klabu ili kuimarisha misingi yake, kuleta utulivu wa wafanyakazi na hatimaye kuungana na utamaduni wa kuwafunza RE Virton, kupitia akademi yake cha Vijana," Taarifa ya R.E Virton ilisoma.

Haya yanajiri wiki chache tu baada ya kiungo huyo mwenye kiwango cha juu kuwaaga The Blues. Mapema mwezi huu, Kante alimaliza ushirikiano wake wa miaka 7 na Chelsea na kuhamia kwa mabingwa wa Saudi Arabia, Al-Ittihad.

Hatua ya kununua klabu hiyo yenye maskani yake karibu na Luxembourg, Ubelgiji inaonyesha kuwa mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 32 amechagua kutumia sehemu ya mapato atakayopata nchini Saudi Arabia kuendesha klabu ya soka.

Royal Excelsior Virton iko katika harakati za kutafuta kurejeshewa leseni yake ya kitaaluma, na itacheza katika Divisheni ya 1 ya Kitaifa ya Ubelgiji msimu ujao.