Rasmi! Raheem Sterling ajiunga na The Blues kutoka Manchester City

Tayari amejiunga na kikosi cha Chelsea nchini Marekani kwa ajili ziara ya matayarisho ya msimu.

Muhtasari

•Sterling alijiunga na klabu hiyo ya London kutoka Manchester City kwa uhamisho uliogharimu Pauni Milioni 47.5 (Ksh 6.7B).

•Mshambuliaji huyo atang'ang'ania nafasi yake katika kikosi cha kwanza cha Chelsea na Mjerumani Timo Werner.

baada ya kujiunga na Chelsea kutoka Manchester City
Mshambuliaji Raheem Sterling baada ya kujiunga na Chelsea kutoka Manchester City
Image: TWITTER// CHELSEA

Klabu ya Chelsea imetangaza usajili wa mshambuliaji matata wa timu ya taifa ya Uingereza Raheem Sterling.

Sterling alijiunga na klabu hiyo ya London kutoka Manchester City kwa uhamisho uliogharimu Pauni Milioni 47.5 (Ksh 6.7B).

Mshambuliaji huyo tayari amejiunga na wachezaji wengine wa kikosi  cha Chelsea nchini Marekani kwa ajili ziara ya maandalizi ya msimu.

Taarifa iliyotolewa na Chelsea ilithibitisha kuwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27 altia saini mkataba wa miaka mitano ambao utamuweka katika klabu hiyo hadi 2027.

Baada ya kukamilisha uhamisho wake, mzaliwa huyo wa  Jamaica aliweka wazi kwamba anafurahia sana kurejea London ambako alilelewa.

"London ni nyumbani kwangu na ambapo yote yalianza kwangu, na inashangaza kuwa sasa nina nafasi ya kucheza mbele ya marafiki na familia wiki kila wiki katika Stamford Bridge. Natarajia sana kukutana na mashabiki huko hivi karibuni," Alisema Sterling.

Hii ilikuwa baada ya kuwaaga washika dau wote wa Manchester City ambao wamekuwa sehemu ya familia yake kwa miaka saba iliyopita.

"Ninashukuru kwa panda- shuka zote. Kwa vile ni nyakati za kushuka ambazo kwa wakati fulani zimejaribu nguvu na azimio langu na kuniwezesha kusimama hapa mbele yako kama toleo langu bora. Nilifika Manchester nikiwa na umri wa miaka 20, Leo naondoka kama mwanaume," Sterling alisema katika taarifa yake ya Jumatano.

Mshambuliaji huyo atang'ang'ania nafasi yake katika kikosi cha kwanza cha Chelsea na Mjerumani Timo Werner.