Tutafanya 'tuwezalo kumsajili' tena Messi- Rais wa Barcelona Joan Laporta

Rais wa Barcelona Joan Laporta anasema klabu hiyo ni "nyumba" ya Messi huku wakitarajia kumsajili tena fowadi huyo.

Muhtasari

•Mkataba wa Muargentina huyo katika klabu ya Paris St-Germain unamalizika mwezi Juni, huku ripoti zikimhusisha na Saudi Arabia.

•Laporta alisema kumekuwa na "mazungumzo mazuri" kati ya wawili hao na kwamba alimpongeza Messi kwa kushinda Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka jana.

Image: BBC

Rais wa Barcelona Joan Laporta anasema klabu hiyo ni "nyumba" ya Messi huku wakitarajia kumsajili tena fowadi huyo msimu huu wa joto.

Mkataba wa Muargentina huyo katika klabu ya Paris St-Germain unamalizika mwezi Juni, huku ripoti zikimhusisha na Saudi Arabia.

Lakini katika mahojiano na shirika la utangazaji la Uhispania TV3, Laporta alisema Barcelona inaweza kushindana na mtu yeyote kuwania saini ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35.

"Historia inatuunga mkono, hisia ni kali sana, tuna mashabiki milioni 400 duniani kote pia," alisema.

Messi aliondoka kwa wababe hao wa Catalan miaka miwili iliyopita baada ya miaka 21 katika klabu hiyo lakini amekuwa na wakati mgumu katika misimu yake miwili nchini Ufaransa, huku mashabiki wakimzomea baada ya ushindi wao wa 5-0 dhidi ya Ajaccio wikendi.

Laporta alisema kumekuwa na "mazungumzo mazuri" kati ya wawili hao na kwamba alimpongeza Messi kwa kushinda Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka jana.

"Yeye ni mchezaji wa Paris St-Germain na tunapaswa kusubiri hadi mwisho wa msimu, hadi umalizike, na ndipo tunaweza kuzungumza kwa utulivu zaidi kuhusu hili," Laporta aliongeza.

"Kwa heshima zote kwa Saudi Arabia, Barca ni Barca, na ni nyumbani."

Matamshi hayo yanakuja baada ya Barcelona kushinda taji lao la kwanza la La Liga ndani ya miaka minne kwa ushindi wa 4-2 dhidi ya Espanyol Jumapili.

Laporta alionekana kujizuia zaidi kuliko wakati wa usiku wa manane wa Twitch baada ya ushindi huo, ambapo anaripotiwa kusema kuwa klabu hiyo itafanya "kila linalowezekana" kumsajili Messi.