Rais Mustaafu Moi alazwa ICU

MOI
MOI
Rais Mtaafu Daniel Moi amelazwa katika Nairobi Hospital kwenye nchumba cha wagonjwa mahututi chini majuma mawili baada ya kuruhusiwa kurejea nyumbani kutoka hospitali hiyo.

Madaktari katika hospitali hiyo waliambia The Star kuwa rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 95 alikimbizwa hospitalini siku ya Alhamisi wiki iliyopita kutoka boma lake la Kabarnet Gardens, Nairobi.

“Ana matatizo ya njia kupumua. Ana ugumu wa kupumua,” daktari ambaye hakutaka jina lake litajwe aliambia The Star alipoulizwa ugonjwa uliokuwa ukimsumbua Moi.

Katibu wa habari wa Moi, Lee Njiru, ambaye yuko katika boma la Moi la mashambani katika Kaunti ya Nakuru, alipuuzilia mbali ripoti kwamba Moi amelazwa.

"Rais Mustaafu Moi anapumzika Kabarnet Gardens. Aliondoka hospitalini majuma mawili yaliopita. Hajarejeshwa hospitalini tena lakini anapumzika nyumbani kwake,” Msemaji huyo wa miaka mingi wa Moi alisema.

Hata hivyo, Katibu mkuu wa Kanu Nick Salat alithibitisha kuwa Moi amelazwa hospitalini “ kwa uchunguzi wa kawaida lakini sio chumba cha wagonjwa mahututi ICU”.

Salat alisema kwamba Moi alikuwa amekwenda hospitalini siku mbili zilizopita kwa uchunguzi wa kiafya ambao ulikuwa umepangwa mara ya mwisho alikuwa hospitalini.

Aliongeza kuwa,“Mzee amezeeka na kila siku akiwa salama tumashukuru Mungu. Sisi sote tuna watu wenye umri kama huo na kila mara wanaenda hospitalini”.

Moi aliruhusiwa kuondoka hospitalini Oktoba tarehe 16 na kupelekwa kwa boma lake la Kabarnet Gardens, lililoko kilomita chache kutoka Nairobi Hospital. Mwezi Machi mwaka 2018, Moi alisafiri nchini Israeli kwa kile familia ilitaja kama tatizo la goti.

Januari tarehe 27, 2017 alifanyiwa upasuaji wa goti katika hospitali ya Aga Khan mjini Nairobi.

Moi alichukuwa hatamu za uongozi wa taifa la Kenya baada ya kifo cha mawanzilishi wa taifa hayati mzee Jomo Kenyatta mwaka 1978. Kabla ya hapo Moi ambaye alikuwa wakati mmoja mwalimu wa shule ya msingi, alikuwa amehudumu kama makamu wa rais wa Kenyatta kati ya mwaka 1967 – 1978.