Ni mjinga! Gidi amkashifu jamaa aliyetumia milioni 21 kufanyiwa upasuaji wa kuongeza urefu

Mtangazaji huyo alidokeza kuwa wanawake wengi hufuata pesa bali sio urefu.

Muhtasari

• Gidi alisema kuwa uamuzi wa jamaa huyo ulikuwa wa kijinga kwani urefu sio jambo kuu ambalo wanawake huzingatia kwa wanaume.

•Gibson alifichua jinsi ambavyo amekuwa na shida kupata mwanamke aliye tayari kukubali urefu wake.

Gidi Ogidi

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Gidi Ogidi amemkosoa mwanaume wa Marekani ambaye alitumia dola 165,000 (Ksh 21.5M) kufanyiwa upasuaji wa kuongeza urefu wake ili awavutie wanadada.

Akizungumza wakati wa kipindi cha siku ya Ijumaa, Gidi alisema kuwa uamuzi wa jamaa huyo, Moses Gibson ulikuwa wa kijinga kwani urefu sio jambo kuu ambalo wanawake huzingatia kwa wanaume wa kuchumbiana nao.

Alidokeza kuwa wanawake wengi kote ulimwenguni hufuata pesa ambazo jamaa huyo kutoka Minneapolis tayari alikuwa nazo.

"Gibson ni mjing! Ni mjinga kwa sababu twajua kwamba, kitu kimoja ambacho wanadada huwa wanapenda (na sio kwa ubaya wanadada msinichukulie vibaya), sio urefu, sio kitambi chako, sio nguo yako, sio jinsi unavyonukia, ni pesa,"  Gidi alisema.

Mtangazaji huyo mahiri alimwambia Gibson, "Tayari uko na shilingi milioni 21 za Kenya. Badala ya kupatia wanadada wakupende, wewe unaenda kukatwa miguu. Badala ya kutumia pesa hizo ili wanawake wakupende, wewe unaenda kupatia daktari mmoja ukatwe miguu na unaambiwa kwamba kuna madhara."

Hivi majuzi, mwanaume mmarekani kwa jina Moses Gibson alitumia Sh milioni 21 kukuza urefu wake kwa inchi 5 zaidi.Jamaa huyo wa kutoka Minneapolis alifanyiwa upasuaji mara mbili ili kukua kutoka 5'5 hadi 5'10. Inasemekana alikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu urefu wake na hivyo kuchukua hatua hiyo.

Gibson alifichua jinsi ambavyo amekuwa na shida kupata mwanamke aliye tayari kukubali urefu wake. Alisema aliaibishwa sana na watu kwa sababu ya kimo chake kifupi kutoka akiwa na umri mdogo.

Jamaa huyo mwenye umri wa miaka 41 alijaribu kila aina ya dawa ambazo ziliahidi matokeo makubwa hata kufikia hatua ya kutafuta mganga kwa tamaa ya kuwa mrefu. 

Gibson nusura apoteze tumaini wakati alipogundua upasuaji wenye uchungu unaohusisha kuvunja mifupa mingi. 

Alifanya upasuaji mara mbili. Upasuajii wa kwanza alipata inchi tatu zaidi mwaka wa 2016 na sasa anatumai kufikia urefu wa lengo lake la 5ft 10in ifikapo Juni baada ya kufanyiwa upasuaji wa pili wa kuongeza inchi mbili.

Ametumia jumla ya $160,000 kwa upasuaji huo unaoelezewa kuwa mkali. Hata hivyo anasisitiza kuwa amefurahishwa na matokeo.