Gidi asherehekea ‘ndoa’ yake ya miaka 16 na Ghost Mulee, afichua siri ya ushirikiano wao mzuri

Mtangazaji wa Radio Jambo Gidi Ogidi amesherehekea ushirikiano wake mzuri na mwenzake Jacob ‘Ghost’ Mulee.

Muhtasari

•Gidi alibainisha kuwa ushirikiano wa utangazaji wa redio ni kama ndoa, akidokeza watangazaji-wenza wanapaswa kufahamiana na kukabiliana na kila mmoja.

•Pia alichukua fursa hiyo kuwatambua mamillioni ya mashabiki wao na kuwathamini kwa sapoti yao inayoendelea.

studioni.
Watangazaji Ghost Mulee na Gidi Gidi studioni.

Huku ulimwengu mzima ukiadhimisha Siku ya Redio Ulimwenguni mnamo Jumanne, mtangazaji tajika wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Joseph Ogidi almaarufu Gidi Gidi amesherehekea ushirikiano wake na mtangazaji mwenzake Jacob ‘Ghost’ Mulee.

Katika chapisho kwenye kurasa zake za mitandao yake ya kijamii, mwanamuziki huyo wa zamani alibainisha kuwa ushirikiano wa utangazaji wa redio ni kama ndoa akidokeza kwamba watangazaji-wenza wanapaswa kufahamiana na kukabiliana na kila mmoja, jambo ambalo yeye na Ghost wamefanikiwa kufanya vizuri kwa zaidi ya muongo mmoja na nusu.

"Ushirikiano wa utangazaji wa redio ni kama ndoa, huwezi kutoboa ikiwa huwezi kukabiliana na ujinga wa kila mmoja!," Gidi Ogidi alisema kupitia mtandao wa Facebook.

Aliambatanisha taarifa yake na picha nzuri zake na Ghost wakiwa studio.

"Imekuwa miaka 16 ya redio ya asubuhi na rafiki yangu Ghost Mulee," aliongeza.

Mtangazaji huyo mahiri wa redio pia alichukua fursa hiyo kuwatambua mamillioni ya mashabiki wao na kuwathamini kwa sapoti yao inayoendelea.

“Asanteni kwa mashabiki wetu wote kwa kusikiliza. Heri ya Siku ya Redio Duniani,” aliandika.

Ni wazi kwamba kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo ndicho kipindi kikubwa zaidi cha redio cha asubuhi nchini Kenya.

Utafiti wa mwaka jana uliofanywa na shirika la IPSOS ulithibitisha kuwa shoo hiyo ambayo hupeperushwa kila siku za wiki kutoka saa kumi na mbili asubuhi hadi saa nne asubuhi ndiyo shoo maarufu zaidi ya asubuhi humu nchini. 

Kipindi hiki hupeperushwa na mabingwa wawili wa utangazaji, Joseph Ogidi almaarufu Gidi na Jacob Ghost Mulee ambao wamekuwa na muungano nzuri kwa takriban miaka kumi na sita ambayo wamefanya kazi pamoja.

Mwaka jana, mtangazaji Ghost' Mulee aliambia mwanahabari Samuel Maina kuwa kufanya kazi kama mtangazaji mwenza wa Gidi imekuwa ni safari nzuri ya kufarahisha.

Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Harambee Stars alibainisha kuwa ni mara chache tu  ametofautiana na Gidi kwa takriban miaka kumi na mitano iliyopita ambayo wamekuwa wakifanya kazi pamoja.

"Tumefanya kazi vizuri kwa miaka kumi na nne bila wasiwasi wowote.  Hakuna kukorofishana, huwa ni masuala ya kazi, kama kuna tofauti huwa za kikazi na baada ya pale tunatoka tunaenda zetu," alisema.

Ghost alilinganisha uhusiano wake wa kikazi na Gidi na ndoa imara.

Hata hivyo, alikiri kuwa kama ndoa nyingine yoyote, hakujakosa changamoto katika 'ndoa' yake na mtangazaji huyo. Alibainisha kuwa mara zote Gidi huwa tayari kumrekebisha kila anapokosea kazini.

"Ni ndoa ambayo huwezi kuiacha isipokuwa uamue hivyo. Tumekaa kwa hii ndoa miaka kumi na minne. Imekuwa ni changamoto. Gidi ana haiba tofauti na yangu. Lakini nampenda kwa sababu tukifanya naye kazi, unapata saa zingine mimi ni mtu wa mzaha, nikitoka laini ananirejesha kama mwalimu mkuu," alisema.

Ghost pia alizungumzia kitengo maarufu kwenye kipindi chao 'Patanisho' na kusema kuwa inawapa furaha nyingi kusaidia watu kurudiana.

"Ni raha yetu waliokosana wakiweza kupatana na kurudiana. Hakuna haja ya kukaa na kinyongo moyoni. Kama umekosea mtu muombe msamaha. Kama amekukosea nawe kubali msamaha," alisema.