Tukio la kutisha kwenye Kilimanjaro lililomfanya Gidi kuapa kutojaribu tena kupanda milima

“Kupanda milima si jambo rahisi; lazima uwe tayari kimwili na kiakili," Gidi alisema.

Muhtasari

•Gidi alisimulia tukio la kutisha ambalo alishuhudia akipanda Mlima Kilimanjaro kwa mara ya pili miaka mingi iliyopita.

•Mtangazaji huyo alisema alijisikia vizuri baada ya kurejea kambini. Hata hivyo, aliapa kutojaribu tena kupanda milima.

amesimulia tukio la kutisha kwenye Mlima Kilimanjaro
Mtangazaji Gidi amesimulia tukio la kutisha kwenye Mlima Kilimanjaro

Mtangazaji mahiri wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo, Joseph Ogidi almaarufu Gidi amezungumza kuhusu matukio yake ya kupanda milima.

Mwimbaji huyo wa zamani amesimulia hadithi yake baada ya mpanda milima wa Kenya, Joshua Cheruiyot Kirui kupoteza maisha yake alipokuwa akijaribu kufika kilele cha mlima mrefu zaidi duniani, Mlima Everest bila oksijeni ya ziada.

Katika hadithi yake, Gidi alifichua kwamba amewahi kupanda Mlima Kenya na Mlima Kilimanjaro. Hata hivyo alikiri kwamba kupanda milima si jambo rahisi.

“Kupanda milima si jambo rahisi; lazima uwe tayari kimwili na kiakili. Hata hivyo, ajali hutokea. Kwa upande wa Cheruiyot, kwa bahati mbaya alianguka kwenye shimo. Nimepanda Kilimanjaro hadi kilele cha Uhuru mara mbili, na Mlima Kenya hadi kilele cha Lenana mara moja,” Gidi alisema.

Alizungumza kuhusu jamba mbaya zaidi lililowahi kutokea katika shughuli zake za upandaji mlima na kusimulia tukio la kutisha ambalo alishuhudia wakati akipanda Mlima Kilimanjaro kwa mara ya pili miaka mingi iliyopita.

Tukio langu mbaya zaidi lilikuwa ni kupanda kwa mara ya pili Mlima Kilimanjaro. Nilichoka sana mita chache kutoka kilele na niliamua kupumzika. Nilipoteza mawasiliano na kikundi changu, ambacho kilikuwa mbele sana.

Mmoja wa wasimamizi aligundua kuwa nilikuwa namekumbwa na usingizi akanishika chini huku akinionya kuwa nikithubutu kulala hapo ndio utakuwa mwisho wangu. Wapandaji wengi wamekufa karibu na sehemu hiyo. Nilijitahidi kutembea na hatimaye kufika kileleni.

Hapo ndipo nilipojifunza kuhusu ugonjwa wa milimani, ambapo unasikia kizunguzungu, usingizi, na uchovu, na kitu pekee unachoweza kufanya ni kushuka kwenye urefu haraka uwezavyo,” alisimulia.

Mtangazaji huyo mahiri alisema kuwa alijisikia vizuri baada ya kurejea kambini. Hata hivyo, baada ya tukio hilo aliapa kutojaribu tena kupanda milima.

"Walakini, ni uzoefu wa kuridhisha ambao unaweza kujaribu katika maisha yako. RIP Cheruiyot Kirui,” alisema.

Siku ya Jumatano, familia ya Cheruiyot Kirui ilitangaza kwamba mwili wa mkweaji huyo Mkenya ungesalia Mlima Everest na hautarejeshwa kwani ni shughuli hatari.