Jinsi kidole cha Nadia Mukami kilivyomzuia Arrow Bwoy kumchumbia Marekani

"Nilipaswa kumchumbia akiwa Marekani. Lakini niliona kidole chake kilikuwa kidogo sana," Arrow Bwoy alisema.

Muhtasari

•Arrow Bwoy alifichua kwamba alikuwa amepanga kila kitu ila hatimaye mpango wake huo ukagonga mwamba.

•Nadia alidokeza kuwa katika siku za nyuma walikuwa wamepanga harusi ya kitamaduni ambayo mwishowe haikufanikiwa.

Image: INSTAGRAM// NADIA MUKAM

Mwimbaji wa Kenya Ali Yusuf almaarufu Arrow Bwoy amefichua kwamba alipanga kumvisha pete ya uchumba mpenzi wake Nadia Mukami wakati wa ziara yake ya kimuziki nchini Marekani mwaka wa 2021.

Wakati wa mahojiano na mtangazaji Massawe Japanni siku ya Jumatatu, Arrow Bwoy alifichua kwamba alikuwa amepanga kila kitu na kuweka mikakati yote ila hatimaye mpango wake huo ukagonga mwamba.

"Nilipaswa kumchumbia (Nadia Mukami) wakati akiwa Marekani. Lakini niliona kidole chake kilikuwa kidogo sana. Nilikuwa na pete mfukoni, nilikuwa nikiangalia kidole chake kila wakati," Arrow Bwoy alisimulia.

Baba huyo wa mtoto mmoja alieleza kwamba kufuatia hali iliyojitokeza, hakuwa na budi ila kurejesha pete ile.

“Ilinibidi niirudishie pete. Wakati wa kurudishga, tayari alikuwa amesharejea Kenya, mimba nayo ilikuwa inamkimbiza," alisema.

Wapenzi hao walikuwa wakijibu swali kuhusu mipango yao ya harusi.

Arrow Bwoy alibainisha kwamba kumuoa rasmi mzazi huyo mwenzake ni jambo ambalo limo akilini mwake.

"Wakati mwafaka unakuja, inaweza kuwa mwaka huu, kesho ama mwaka ujao," alisema.

Nadia alidokeza kuwa katika siku za nyuma walikuwa wamepanga harusi ya kitamaduni ambayo mwishowe haikufanikiwa.

"Pia tulikuwa tunapanga harusi ya kitamaduni lakini tukakosana na tukaachana kwa muda," alisema.

Alisema tayari alikuwa amemuarifu baba yake kuhusu mpango huo.

Katika mahojiano hayo, wapenzi hao wamlifichua kuwa walitengana kwa kipindi cha takriban wiki mbili mwaka jana.

Wawili hao walieleza kwamba walienda njia tofauti kufuatia mzozo wa kinyumbani huku Nadia akifichua mumewe aliondoka nyumbani baada ya wao kuzozana.

"Niliondokea pressure kidogo. Unajua ukiwa na mwenzako alafu uone mambo imeenda mrama, wakati mwingine ni vizuri kujipatia nafasi," Arrow Bwoy alijitetea.

Alidokeza kuwa kiburi kati yao kiliwafanya wasikae chini na kutatua mzozo wao.

Nadia alikiri kwamba alizidiwa na mambo mengi ambayo yaliyomkumba baada ya kujifungua mapema mwaka jana.

"Baada ya kujifungua na najaribu kujiinua. Ilikuwa ngumu kwangu. Nilipitia msongo wa mawazo baada ya kujifungua," Nadia alisema.

Wanandoa hao walifichua kwamba baada ya takriban wiki mbili, Arrow Bwoy alirudi nyumbani na wakasuluhisha mzozo wao.

"Tulikaa chini tukaongea. Hakuomba msamaha. Alikuja tu akauliza mtoto ako aje," Nadia Mukami alisema.

Arrow Bwoy alisema, "Nilisikia vitu anapitia nikaona sio rahisi. Nikaona nitulie.Sikuwa nampatia wakati wa kuketi chini."