"Sioni sababu ya kumuua" DJ Fatxo afunguka uhusiano wake halisi na marehemu Jeff Mwathi

"Jeff alikuwa rafiki yangu. Sioni sababu yangu kumuua," alisema.

Muhtasari

•DJ Fatxo alisema marehemu alikuwa rafiki yake na kubainisha hakuwa na sababu yoyote ya kumdhuru.

•Alibainisha kuwa hakuwa akiwasiliana na Jeff kwa simu hadi mwaka wa 2023 ambapo alihitaji marehemu amfanyie kazi.

DJ Fatxo ndani ya studio za Radio Jambo
Image: RADIO JAMBO

Mwimbaji wa nyimbo za Mugithi Lawrence Njuguna almaarufu DJ Fatxo amefunguka kuhusu uhusiano wake halisi na marehemu Jeff Mwathi.

Akizungumza wakati wa mahojiano na Massawe Japanni, msanii huyo ambaye hivi majuzi aliondolewa madai ya mauaji ya Jeff  alisema marehemu alikuwa rafiki yake na kubainisha hakuwa na sababu yoyote ya kumdhuru.

"Jeff alikuwa rafiki yangu. Sioni sababu yangu kumuua," alisema.

Hata hivyo, aliweka wazi kwamba urafiki wao haukuwa wa karibu bali ulikuwa wa kikazi.

Hatukuwa na urafiki wa karibu. Ilikuwa tukipatana tu wakati nanunua viatu," alisema. 

DJ Fatxo alifichua kuwa alikuja kujuana na kijana huyo wa miaka 23 mwaka wa 2021 kupitia rafikiye mwanamke ambaye alikuwa akimuuzia viatu. Wakati huo alikuwa akivuma kutokana na nyimbo maarufu alizokuwa ameachia.

"Jeff alikuwa na duka la viatu. Napenda mambo na fashion, nilienda pale nikapata mwanadada kwa jina Faith Mutanu. Sikujua duka ni kwa Jeff. Nilikuwa nimenunua viatu vya zaidi ya laki moja," Fatxo alisimulia.

Aliongeza, "Jeff alisema shukran ati nimekuwa nikimpromote sana. Sikuacha kuwa customer wake. Tulipopatana alipiga picha na mimi. Hapo akaniambia Samidoh ni mjomba wake. Mimi nikatupilia mbali kwa kuwa sikuona mengine ya kuzungumza naye."

Alisema Jeff alimpata pale dukani mara kadhaa baada ya mkutano wa kwanza ila hawakuwahi jenga urafiki wa karibu.

Jeff baadaye alimwambia  mwimbaji huyo kuhusu kazi yake ya kupamba maduka kama alivyokuwa amepamba duka lake.

"Aliniona mara nyingi. Alikuwa na mazoea ya kupiga picha. Aliponipata siku ingine akaniambia nikitaka kutengeneza duka la viatu nimwambia kwani yeye ndiye alitengeneza ile yake," Fatxo alisema.

Alibainisha kuwa hakuwa akiwasiliana na Jeff kwa simu hadi mwaka wa 2023 ambapo alihitaji marehemu amfanyie kazi.

Hata hivyo, aliweka wazi kwamba marehemu alikumbana na kifo chake kama bado hajamfanyia kazi yoyote.