'Mama Mdogo alinikasirikia niliposhindwa kumlipia mwanawe karo nikiwa na miaka 16'

Kijana huyo wa miaka 21 kutoka Baba Dogo Nairobi alisema kwamba mtoto wa babake mdogo alikuwa anajiunga kidato cha kwanza 2019 na mama mdogo alimuomba kumsaidia na karo lakini hakuwa nayo.

Muhtasari

 
• “Huo wakati nilikuwa nimetoka nyumbani kuna mtu nilikuwa nafanyia kazi kwa boma… niliongea na bosi wangu nikamuuliza kama ana uwezo wa kusaidia huyu mtoto kumsaidia kumsomesha,"

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi cha Patanisho kwenye stesheni ya Radio Jambo na manahodha Gidi na Ghost, kijana wa miaka 21 kwa jina Victor Jaoko kutoka maeneo ya Baba Dogo Nairobi alitaka kupatanishwa na mamake mdogo, mke wa ndugu ya babake.

Jaoko alisema kwamba uhusiano wake na mama mdogo Iska Jombo mwenye umri wa miaka 40 ulianza pale alipomtaka kumsaidia kumlipia karo mtoto wake ambaye alikuwa anajiunga kidato cha kwanza mwishoni mwa mwaka 2019.

Jaoko alisema kwamba kipindi hicho alikuwa na miaka 16 na hakuwa na kazi licha ya kuwa alikuwa Nairobi lakini mama mdogo alidhani kwamba mtu akiwa Nairobi ana pesa za kuweza kumlipia karo mtoto wake.

Hata hivyo, kijana huyo alisema kwamba kilichomponza ni matumaini aliyowacha kwa mama mdogo kwa kumuahidi kwamba kuna mtu ambaye alikuwa anategemea kuzungumza na yeye kumfadhili mtoto huyo shuleni lakini baadae mtu huyo akaghairi lakini mama mdogo hakuweza kuelewa hili.

“Huo wakati nilikuwa nimetoka nyumbani kuna mtu nilikuwa nafanyia kazi kwa boma… niliongea na bosi wangu nikamuuliza kama ana uwezo wa kusaidia huyu mtoto kumsaidia kumsomesha, niliporudi kuongea na yeye akasema hawezi kwa sababu ana watoto wake… kutoka hapo mambo yakaanza hivyo tukakosana, hata nikimpigia simu hashiki…” Jaoko alisema.

“Katika hiyo miaka 5 nimejaribu kumpigia simu hashiki, nikimtafuta whatsapp hanijibu… si kama zamani tulipokuwa na uhusiano… niliuliza baba mdogo kwa nini shangazi hashiki simu… nilikuwa nataka mnipatanishe na yeye niweze kuridhika tukuwe tunaongea na yeye… nikiwa huku wakati uhusiano ulikuwa mzuri alikuwa ananitumia kitu kutoka nyumbani lakini tangu hivyo aliacha…” alisema.

Kwa upande wake Iska Jombo alipopigiwa simu, alianza kwa kucheka kisha akamwambia Jaoko kwamba si kwa ubaya kwa kukosa kushika simu yake wala kujibu meseji zake WhatsApp.

“Haikukuwa makosa sana, wewe ndio ulichukua kama makosa lakini mimi sikuchukua kama makosa, hata nimeshangaa leo ukisema kwamba ulinikosea. Kwanza wewe ndio uliweka namba yangu blacklist, nilikupigia simu haingii nikasema niache tu,” Iska alisema.