Wanaume ni waaminifu sana, wanawake ndio husumbua- Mtangazaji Gidi

“Mimi kwa mfano, kinyozi alianza kuninyoa nikiwa shule ya upili ndiye ananinyoa mpaka leo. Huwa anahama namfuata!" Gidi alisema.

Muhtasari

•Gidi alibainisha kuwa pindi wanaume wanapofanya uamuzi, wao sio tu waaminifu katika ndoa tu, bali pia kwa vilabu vyao vya soka na vinyozi mara.

•Mtangazaji huyo mahiri alidai kuwa wanaume sio watu wasio waaminifu bali ni wanawake ambao huzua usumbufu.

Gidi Ogidi
Image: RADIO JAMBO

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo, Joseph Ogidi almaarufu Gidi Gidi amewatetea wanaume kuhusu suala la uaminifu katika ndoa.

Katika mahojiano ya kipekee na Radio Jambo, mwimbaji huyo wa zamani wa kundi la ‘Gidi Gid Maji Maji’ alibainisha kuwa wanaume ndio viumbe waaminifu zaidi duniani.

Alisema wanawake huwa wanakosea kwa kutilia shaka uaminifu wa wanaume, akibainisha kuwa pindi wanapofanya uamuzi, wao sio tu waaminifu katika ndoa tu, bali pia kwa vilabu vyao vya soka na vinyozi mara.

"Kitu kimoja kuhusu wanaume ambacho watu wanafaa kujua, mara unapoamua kuhusu jambo fulani, hasa mambo ya mpira,  kinyozi na ata mambo ya ndoa, basi umeamua," Gidi alisema.

Aliongeza “Hata nashangaa kwa nini wanawake wengi huwa wanasema eti ooh, “wanaume kwa kawaida ni waaminifu kwa timu yao ya soka, lakini hawawezi kuwa waaminifu kwa wanawake.. ooh , nini na nini..” apana, wanaume ni waaminifu kila mara.”

Gidi alitoa mfano wa yeye mwenyewe akibainisha kuwa amekuwa mwaminifu kwa klabu anayoipenda zaidi ya Arsenal tangu alipoanza kuishabikia zaidi ya miongo mitatu iliyopita.

Isitoshe, mtangazaji huyo pia alifichua kuwa kinyozi aliyeanza kumnyoa wakati akiwa shule ya upili anamnyoa hadi leo, na hajawahi kubadilisha tangu wakati huo.

“Mimi kwa mfano saa hizi, kinyozi alianza kuninyoa nikiwa shule ya upili ndiye ananinyoa mpaka leo. Huwa anahama, alianza na town, akaenda Hurlingam, anaenda wapi, lakini mimi humfuata hadi leo, Huyo ni kinyozi wangu mpaka leo, uaminifu,” alisema.

Aliongeza, “Timu ya soka, nilianza kuisaidia Arsenal zaidi ya miaka 30 iliyopita. Mpaka wa leo bado nasupport Arsenal. Kwa hivyo, wanawake wanafaa kujua wanaume ni watu waaminifu sana.”

Mtangazaji huyo mahiri alidai kuwa wanaume sio watu wasio waaminifu bali ni wanawake ambao huzua usumbufu.

“Ni wanawake hutusumbua. Kweli ama uongo? . Wanawake ndio husumbua. Lakini wanaume ni waaminifu sana,” alisema.

Gidi aliyasema hayo huku akimkosoa mtangazaji mwenzake Jacob ‘Ghost’ Mulee kwa kuacha kuisapoti timu yake aliyoipenda sana, Arsenal.

“Kwa hivyo, hilo swali umeulizwa, mimi ni mwaminifu kwa Arsenal, tangu wakati nilianza. Mimi pia ni shabiki wa Lionel Messi tangu enzi, na Freddie Ljungberg, pamoja na Thiery Henry, ni wachezaji wangu pendwa wakati wote. Sasa hivi pale Arsenal , ni Odegaard, mtu wangu. Na Rice,,” Gidi alisema.

Ghost alidai kuwa aliacha kuishabikia klabu ya Arsenal baada ya kubaini kuwa klabu hiyo ingeweza kumuua kwa msongo wa mawazo kwa kuwa haikuwa ikishinda chochote.