Wanyama kupambana na Salah katika michuano ya kufuzu AFCON 2021

afcon 2021
afcon 2021
Harambee Stars watachuana na Misri, Togo na visiwa vya Comoro katika kundi G la michuano ya kufuzu kwa AFCON mwaka wa 2021.

Hii itakua mara ya kwanza kwa Stars kupambana na Pharaohs katika kufuzu kwa AFCON lakini wameshawahi kupambana na Togo na visiwa vya Comoro.

Kenya ilishiriki michuano hiyo mwaka huu baada ya kukosa kwa miaka 15 lakini walibanduliwa katika raundi ya kwanza baada ya kupata ushindi mmoja tu dhidi ya Tanzania.

Raundi ya kwanza ya michuano hiyo ya kufuzu itafanyika Novemba tarehe 11. Ni timu mbili tu za juu kwa kila kundi ndizo zitafuzu.

Hata hivyo, Jukwaa liko tayari kwa mechi ya fainali ya AFCON mwaka wa 2019, itakayoandaliwa leo saa nne usiku nchini Misri kati ya Algeria na Senegal. Mlinzi nyota wa Senegal Kalidou Koulibaly atakosa mechi hiyo baada ya kupata kadi ya pili ya njano kwenye kipute hicho katika mechi yao ya nusu fainali waliyoshinda dhidi ya Tunisia.

Senegal wamecheza fainali ya AFCON mara moja huku Algeria wakishiriki mara mbili.

Kwingineko, Amaju Pinnick wa Nigeria ameachishwa kazi kama naibu wa rais wa shirikisho la soka barani Afrika na nafasi yake kuchukuliwa na Danny Jordaan wa Afrika Kusini.

Pinnick amehudumu kama naibu rais wa Caf tangu Julai mwaka wa 2018. Hakuna sababu imetolewa ya kubanduliwa kwake na rais wa Caf Ahmad, ambae alitia saini makubaliano na rais wa Fifa Gianni Infantino hapo jana kuidhinisha uteuzi wa katibu mkuu wa Fifa Fatma Samoura kama mjumbe wa Afrika.