Baha asema huenda ujio wa mtoto wake ni kuzaliwa upya kwa marehemu mama yake

Muhtasari

•Tyler alisema ana uhakika kuwa alipo mama yake ana raha kuona hatua kubwa ambayo amepiga kama mwanawe.

•Tyler amesema mpenziwe alionyesha ujasiri mkubwa wakati alipokuwa anajifungua binti wao mapema mwezi huu.

Image: INSTAGRAM// KAMAU MBAYA

Mwigizaji Tyler Kamau Mbaya almaarufu Baha amempongeza mpenzi wake Georgina Njenga kwa kujifungua mtoto wao wa kwanza.

Tyler amesema mpenziwe alionyesha ujasiri mkubwa wakati alipokuwa anajifungua binti wao mapema mwezi huu.

"Nahisi kama kwamba yeye ndiye mtu jasiri zaidi ambaye nimewahi kuona. Alinithibitishia uchungu ambao mama yangu alipitia wakati alikuwa ananizaa hasa kwa kuwa alimleta tena mama yangu katika siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwangu," Baha alisema akiwa katika mazungumzo na Diana Marua.

Mwigizaji huyo wa zamani wa kipindi cha Machachari alisema kuzaliwa kwa bintiye huenda ni kuzaliwa tena kwa marehemu mama yake. 

Tyler alisema ana uhakika kuwa alipo mama yake ana raha kuona hatua kubwa ambayo amepiga kama mwanawe.

"Mahali tu aliko najua ana raha. Labda ata ndiye huyu tunaongelesha. Mimi ni mtu wa kiroho na naamini katika kuzaliwa tena. Labda yupo hapa na anatusikiza," Alisema.

Tyler na mpenziwe walitangaza habari za kuzaliwa kwa mtoto wao wa kwanza pamoja takriban wiki mbili zilizopita.

Wapenzi hao wawili hao walifichua kuwa binti yao alizaliwa mnamo siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Tyler.

Alikuja siku ya  kuadhimisha kuzaliwa kwangu. Tungependa kuwafahamisha nyie kuwa mtoto na mama yake wanafanya vizuri na wanatunzwa hapa hospitalini. Ni hadithi kubwa ya jinsi mambo yalivyotokea.Hatuwezi kusubiri kuwapeleka katika safari yote. Tunawapenda," Tyler alitangaza kupitia Instagram.

Mwigizaji huyo ameapa kuwepo katika maisha ya binti yao na kusawazisha kazi zake na kumshughulikia mtoto.

"Baba yangu alikuwepo, sio eti hakuwa. Ni ile lazima angefanya kazi. Alienda Marekani miaka kumi. Siwezi taka kuweka mtoto wangu katika hali kama hiyo. Nitapambana kuwepo nyumbani na nifanye kazi bado. Heri ikuwe asilimia 50. Tutapatia mtoto wakati mwingi," Alisema Tyler.

Aidha aliweka wazi kuwa yeye na mpenziwe wapo tayari kwa majukumu ya uzazi yaliyo mbele yao.