"Ndoto imetimia!" Vera Sidika ajawa furaha kwa kujaliwa mtoto wa kiume

Walitumia chopa kufichua jinsia ya mtoto wao ambaye hajazaliwa.

Muhtasari

•Wawili hao walifika kwenye karamu hiyo ya siri iliyofanyika Windsor Golf Hotel and Country Club  kwa gari la kifahari aina ya Hammer Limousine.

•Vera alisema kwamba walichagua kutumia chopa kufichua jinsia ya mtoto wao wa pili kwani walitaka kitu cha kipekee.

Image: INSTAGRAM// VERA SIDIKA

Siku ya Alhamisi, wanandoa mashuhuri Vera Sidika na Brown Mauzo waliandaa karamu ya kupendeza ya kufichua jinsia ya mtoto wao wa pili pamoja.

Wawili hao walifika kwenye karamu hiyo ya siri iliyofanyika Windsor Golf Hotel and Country Club  kwa gari la kifahari aina ya Hammer Limousine huku wakiwa wamembeba mtoto wao wa kwanza, Asia Brown.

Walitumia chopa kufichua jinsia ya mtoto wao ambaye hajazaliwa. Watu wachache wa karibu waliokuwa wamealikwa kwenye karamu hiyo waliimba kwa furaha huku chopa akiachia moshi wa bluu kuashiria kwamba mwanasosholaiti huyo mwenye umri wa miaka 33 anatarajia mtoto wa kiume.

"Napiga kelele!! Tunapata Mvulana. Ndoto imetimia. Hatimaye nina mvulana wangu," alisema baada ya jinsia ya mwanawe kufichuliwa.

Vera alisema kwamba walichagua kutumia chopa kufichua jinsia ya mtoto wao wa pili kwani walitaka kitu cha kipekee.

Aidha, alifunguka kuhusu furaha yake kubwa kujua kwamba anatarajia mtoto wa kiume ambaye anaweza kushikamana naye vizuri zaidi kwani binti yake wa kwanza ana uhusiano mkubwa na baba yake Brown Mauzo.

"Asia ni msichana wa baba. Hatimaye tutapata mvulana wa mama. Ninamshukuru Mungu kwa familia yetu inayokua," alisema.

Mauzo kwa upande wake alikiri kuwa alitaka mtoto mwingine wa kike kutokana na uhusiano mzuri kati yake na Asia.

"Lakini kusema kweli, mimi ni mwanaume mwenye raha zaidi. Niko na mimi mdogo wa kufanya mambo ya wavulana na yeye. Namshukuru sana Mungu," alisema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Pia alieleza upendo wake mkubwa kwa familia yake ambayo inaendelea kuwa kubwa.