Familia ya rapa Kunguru yahitaji msaada wa kifedha kumzika

Marehemu atazikwa nyumbani kwao Siaya mnamo Aprili 1.

Muhtasari

•Familia ya Kunguru imeomba msaada wa kifedha ili kukamilisha malipo ya  bili kubwa ya hospitali ambayo ilitokana na matibabu.

• Gidi alifichua kwamba marehemu Kunguru atazikwa mnamo Aprili mosi nyumbani kwao Pap Oriang, katika eneo la Alego, kaunti ya Siaya.

Marehemu Kunguru
Image: HISANI

Familia ya marehemu Eric Onguru almaarufu Kunguru imetoa ombi la msaada wa kifedha ili kukamilisha malipo ya  bili kubwa ya hospitali ambayo ilitokana na matibabu ya mwanamuziki huyo mkongwe.

Familia hiyo pia inahitaji usaidizi ili kumwandalia mwimbaji huyo mazishi ya heshima mnamo  Aprili tarehe mosi.

Hafla ya kuchangisha pesa  imepangwa kufanyika siku ya Jumamosi, Machi 25 katika Kanisa Katoliki la Don Bosco, mtaani Upper Hill, jijini Nairobi. Hafla hiyo itaanza saa nane mchana na kuendelea hadi saa kumi na moja jioni.

"Kwa M-pesa, tafadhali tumia Paybill: 8373428, Nambari ya Akaunti: Jina Lako," familia ilisema kwenye bango.

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo,  Gidi Ogidi alifichua kwamba marehemu Kunguru atazikwa mnamo Aprili mosi nyumbani kwao Pap Oriang, katika eneo la Alego, kaunti ya Siaya.

"Tunaomba msaada wako kwa unyenyekevu ili kulipa bili za hospitali na kumpa mazishi yanayofaa," alisema.

Siku chache zilizopita, Gidi alimuomboleza marehemu Kunguru ambaye aliaga dunia siku ya Jumapili.

Gidi ambaye waziwazi alionekana kushtushwa sana na kifo cha rapa huyo nguli alimuomboleza kama rafiki yake na kuitakia roho yake mapumziko ya amani.

"Eric Onguru almaarufu Kunguru ambaye aliimba 'Baby Don't Go' na Mr Lenny ameaga dunia. Pumzika kwa amani rafiki yangu," Gidi alisema kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii siku ya Jumapili.

Mtangazaji huyo mahiri ambaye pia alikuwa mwimbaji aliendelea kuashiria machungu yake kwa kumpoteza mmoja wa wenzake wa zamani katika tasnia ya muziki.

Kwa mujibu wa meneja wake wa zamani, Kunguru  alifariki siku ya Jumapili mwendo wa saa nane mchana. Marehemu alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Nairobi kwa wiki chache zilizopita.

Meneja huyo wa zamani alieleza kuwa rapa huyo mkongwe amekuwa akilazwa na kuruhusiwa kuenda nyumbani mara kwa mara tangu mwaka wa 2017. Alihusisha ugonjwa wa Kunguru wa muda mrefu na ajali ya barabarabi aliyoipata mwaka wa 2009/10 ambayo iliathiri uti wake wa mgongo.

Kunguru anakumbukwa zaidi kwa nyimbo zake za  maarufu  "I Will Never Let you Go" na "Baby Don't Go", akimshirikisha Mr. Lenny.