"Waeleweni!" Zari awasihi wanaume kuwasamehe wake zao wanapowasaliti kimapenzi

Mwanasoshalaiti huyo amewataka wanaume kuwaelewa wake zao wanapoenda nje ya ndoa.

Muhtasari

•Zari Hassan alibainisha kuwa kwa kawaida wanawake huwasamehe waume zao wakati wanapowasaliti kimapenzi.

•Alisema anapendelea kuwa na mpenzi wake hadi mambo yanaposhindikana na hatimaye wanaamua kutembea njia tofauti.

Zari Hassan
Image: Zari Hassan Instagram

Mwanasoshalaiti maarufu kutoka Uganda  Zari Hassan  amewataka wanaume kuwasamehe wake zao wanapoenda nje ya ndoa.

Akizungumza kwenye video ambayo alichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram Jumanne, mama huyo wa watoto watano alibainisha kuwa kwa kawaida wanawake huwasamehe waume zao wakati wanapowasaliti kimapenzi.

Kufuatia hayo, mzazi mwenza huyo wa staa wa bongo Diamond Platnumz amewasihi wanaume kuwatendea wake zao vivyo hivyo.

"Wanaume ambao wana'cheat. Tunawataka mtupe sapoti, huwa tunawasapoti, tunaelewa, tuko hapo kwa ajili yenu tunasamehe. Kwa hivyo ukipata wanawake wenu waki'cheat, wapatie sapoti sawa pia. Kuwa wa kuelewa, wasamehe, shikamana nao kwa sababu hivyo ndivyo wanawake wanafanya pia," alisema.

Zari hata hivyo aliweka wazi kuwa yeye huwa ha'cheat anapokuwa kwenye mahusiano kwani anapendelea kuwa na mpenzi wake peke yake hadi mambo yanaposhindikana na hatimaye wanaamua kutembea njia tofauti.

Mpenzi huyo wa zamani wa Diamond alizungumza hayo wakati akitetea kauli zake za hivi majuzi ambapo alionekana kuwashauri wanawake kusaliti wapenzi wao kimapeni kwa sababu ya pesa na vitu vingine vya gharama.

Huku akijitetea kufuatia ukosoaji mwingi aliokumbana nao, mama huyo wa watoto watano alidai kwamba hakueleweka.

"Hamukunielewa kabisa. Sijatuma wanawake wenu waende kucheat. Nimesema, mwanaume akikutwa anacheat juu ya matako makubwa, vitu ambavyo havina ata faida. Na wewe umewekwa  kwenye nafasi ya kucheat upewe gari, nyumba, cheat. Kwa nini usifanye hivyo?" Zari Hassan alisema.

Alisema katika nyakati za sasa wanawake wameamka na wanaweza kufanya mambo ambayo wanaume pia wanafanya.

Wikendi, Zari aliwapa wanawake ushauri wenye utata kuwa wanapaswa kusaliti penzi lao wanapopata fursa ya kufanya hivyo kwa ajili ya pesa. Akitetea kauli yake, alisema wanaume wana'cheat kwa sababu za kipuzi.

"Mtoto wa kike, ukipata nafasi ya ku'cheat kwa sababu ya pesa basi fanya hivyo. Hawa wanaume wana'cheat kwa mambo ya kijinga kama mapaja ya rangi ya kahawia, pete za ulimi na makalio makubwa. Saliti penzi kwa nyumba, Saliti penzi kwa kipande cha ardhi, saliti kwa gari la ndoto yako, ndivyo lilivyo," alisema.

Mwanasosholaiti huyo mwenye umri wa miaka  42 hata hivyo alijitenga na mambo aliyowashauri wanawake kuhusu na kusisitiza kuwa yeye huchumbiana kwa ajili ya mapenzi  na hayuko tayari kuwacheza na wanaume tofauti.

"Napenda mapenzi ya kale. Nataka kuwa na mtu wangu na kufanya kila kitu pamoja naye. Mambo madogo kama, kuendesha gari kwa njia ya kuchukua ice cream ya Mc Fluryy. Ni mambo madogo kwangu," Zari alisema.

Zari aliwataka watu walio na wapenzi wa kweli kuwatunza huku akibainisha kwamba sio wengi wakweli wamebaki duniani.