"Wewe ni mbinafsi sana!" Zari amlalamikia mumewe Shakib wiki baada ya kufunga ndoa

Wawili hao walishiriki muda pamoja katika maeneo mbalimbali ya burudani.

Muhtasari

•Zari na mumewe Shakib wanaonekana kuburudika sana huku watoto wake Tiffah Dangote na Prince Nillan wakiwa wamemtembelea baba yao Diamond Platnumz.

• Zari hakuridhika kwani mume huyo wake Mganda hakupongeza mwonekano wake.

Zari na mumewe Shakib
Image: INSTAGRAM// SHAKIB CHAM

Mwanasosholaiti na mfanyibiashara mashuhuri wa Uganda Zari Hassan na mume wake Shakib Cham Lutaaya wanaonekana kuburudika sana pamoja huku watoto wake wawili wadogo, Tiffah Dangote na Prince Nillan wakiwa wamemtembelea baba yao Diamond Platnumz nchini Tanzania kwa ajili ya sikukuu ya Eid.

Tiffah na Nillan walisafiri kwenda Tanzania siku ya Ijumaa na wamekuwa wakishiriki muda mzuri na baba yao. Huku wakifurahia Eid yao katika nchi hiyo  jirani, mama yao amekuwa akifurahia wakati na mumewe.

Siku ya Jumamosi usiku, mama huyo wa watoto watano na mume mwenye umri wa miaka 31 walishiriki muda  pamoja na kujivinjari katika sehemu mbalimbali za burudani nchini Afrika Kusini. Wawili hao ambao pia walikuwa pamoja na marafiki wengine walinasa baadhi ya kumbukumbu nzuri kwenye kamera.

Katika moja ya video alizochapisha, Zari alisikika akisifia mwonekano wa mpenzi huyo wake mdogo kwa umri.

"Usiku wetu, mpenzi unakaa vizuri," Zari alimwambia Shakib.

Shakib ambaye kwa wakati huo alisimama pembeni yake alimshukuru kwa pongezi hizo. Zari hata hivyo hakuridhika kwani mume huyo wake Mganda hakupongeza mwonekano wake.

Huku akikubali shinikizo kutoka kwa mke huyo wake, Shakib alimwambia , "Unaonekana mrembo sana!"

Mwanasosholaiti huyo mwenye umri wa miaka 42 alimjibu kwa utani, "Wewe ni mbinafsi sana!"

Wawili hao kisha waliendelea kushiriki wakati pamoja na kuburudika katika maeneo mbalimbali jijini.  Katika video nyingine, walionekana wakiwa kwenye jumba la sinema wakifurahia sinema pamoja na marafiki zao.

Zari Hassan na Shakib walifunga ndoa ya Kiislamu almaarufu Nikkah wikendi iliyopita baada ya kuchumbiana kwa takribani mwaka mmoja.

Wawili hao walivishana pete usiku wa manane kuamkia Jumatatu katika hafla ya faraghani ambayo ilihudhuriwa na idadi ndogo ya watu.

Katika picha na video hafla hiyo iliyofanyika chumbani ambazo zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii, wapenzi hao walionekana wamevalia Kiislamu kabisa huku wote wakiwa wameketi kwenye mkeka uliotandikwa sakafuni.

Shakib alionekana akiinama kwa goti moja na kumvisha Zari pete ya ndoa kwa furaha kabla ya wawili hao kupigana mabusu huku watu wachache waliohudhuria hafla hiyo wakiwasherehekea kwa makofi.

Vyanzo vya habari kutoka Uganda vilidai kwamba baada ya kuvishana pete katika tukio la faraghani, wawili hao ambao wamekuwa marafiki kwa zaidi ya miaka minne waliweka Nikkah yao bayana kwa wazazi wa Zari.