Wahu astaajabu baada ya binti yake kumdhihaki "wewe ni mzee na mkali!"

Nyakio alitumia umri na ukali wa mwimbaji huyo kama chombo cha kushambulia.

Muhtasari

•Nyakio aliandika barua nzuri akimtakia mama yake heri ya Siku ya Akina Mama na kumweleza jinsi anavyojivunia kuwa bintiye.

•Licha ya sifa zote, Nyakio hata hivyo hakukosa 'kumshambulia' mama yake katika hiyo barua yake.

Wahu na Nyakio
Image: FACEBOOK// WAHU KAGWI

Mwimbaji Wahu Kagwi ameonekana kushangazwa sana na ujumbe wa binti yake Nyakio kwake mnamo siku ya kuwasherehekea kina mama.

Mnamo Jumapili, Mei 15, dunia nzima iliadhimisha siku ya kimataifa ya akina mama ambapo walimwengu waliwasherehekea akina mama muhimu katika maisha yao kwa njia mbalimbali za kipekee.

Binti wa pili wa Wahu na Nameless, Nyakio hakuachwa nyuma katika kumsherehekea mama yake. Aliandika barua nzuri akimtakia mwimbaji huyo heri ya Siku ya Akina Mama na kumweleza jinsi anavyojivunia kuwa bintiye.

"Heri ya Siku ya Akina Mama. Wewe ndiye mama bora zaidi duniani," ilisomeka barua hiyo iliyofichuliwa na Wahu kwenye Facebook.

Licha ya sifa zote, mrembo huyo mwenye umri wa miaka 10 hata hivyo hakukosa 'kumshambulia' mama yake katika hiyo barua yake. Alitumia umri na ukali wa mwimbaji huyo kama chombo cha kushambulia.

“Wewe ni mzee lakini wewe ni bora zaidi, unakuwa mkali sana lakini baba ni mkali zaidi, nimefurahi sana kuwa wewe ni mama yangu. Nyachichi na Wema wako pamoja nami,” ilisomeka barua hiyo.

Wahu alifichua barua hiyo kutoka kwa bintiye kwenye ukurasa wake wa Facebook na kuonyesha mshangao mkubwa.

"Wueh😂😂😂," alisema.

Image: FACEBOOK// WAHU KAGWI

Nyakio ni mtoto wa pili wa wanandoa wanamuziki, Wahu Kagwi na David Mathenge almaarufu Nameless. Wawili hao walibarikiwa na mtoto wa tatu pamoja Oktoba mwaka jana baada ya kusubiri kwa muda mrefu.

Katika taarifa yake, Wahu alisema alifurahia kubeba mtoto wake na alitazamia kwa hamu siku ambayo angekutana naye.

"Tangu nilipojua kuwa nimekubeba nakupenda. Nimependa kila teke ulizopiga na kujigeuza, ziara za daktari ambapo niliona mapigo ya moyo wako, nimependa kukuimbia, kuzungumza nawe ...," alisema.

Wahu aliendelea kusema kuwa alikuwa na wasiwasi na safari hiyo ilimuacha na hisia tofauti.

Alimshukuru Mungu kwa kujifungua vizuri na salama.

"Nimekuwa na wasiwasi, nimesali, na kuhisi mihemko mingi kwa muda wa miezi 9 iliyopita, na hapa ndio sasa... nilipokushika mikononi mwangu kwa mara ya kwanza.

Ni ngumu kuelezea wakati huu, ninachoweza kusema ni Asante, Mungu. Umetuona. #shukrani #asanteMungu #mamaShiru #mamagirls #raisinggirls." alisema.

Wahu alijifungua mtoto wake wa tatu takriban miaka tisa baada ya kujifungua mtoto wake wa pili.