"Hisia bora kabisa!" Gidi ajawa bashasha baada ya kutaza Arsenal ikiilima Man U Emirates

"The Best Experience ever, mabao tatu, pointi tatu, tarehe tatu," Gidi alisema kwa furaha tele.

Muhtasari

•Gidi alishiriki picha za tikiti yake ya kuingia na zingine zilizomuonyesha katika uwanja huo wa London akiwa ameshikilia bendera ya Kenya.

•Bao lililoonekana kumvutia zaidi ni lile la mwisho la mshambulizi Gabriel Jesus katika dakika za mwisho ambalo liliipa Arsenal ushindi wa mabao 3-1.

Image: FACEBOOK// JOE GIDI

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Gidi Ogidi alikuwa katika jiji la London, nchini Uingereza wikendi ambako alitazama mechi ya Arsenal na Manchester United moja kwa moja kwenye uwanja wa Emirates.

Gidi aliondoka Kenya kuelekea nchini Uingereza siku ya Ijumaa na kufika kwa wakati kujiandaa kuhudhuria mechi hiyo iliyojaa mbwembwe.

Siku ya Jumapili, kabla tu ya mechi hiyo kung’oa nanga, alishiriki picha za tikiti yake ya kuingia na zingine zilizomuonyesha katika uwanja huo wa London akiwa ameshikilia bendera ya Kenya.

"Tuko tayari! COYG,” Alisema kupitia Facebook dakika chache kabla ya mechi.

Wakati mechi ikiendelea, alipakia picha zaidi za mashabiki waliokusanyika uwanjani na video zake akishangilia wakati timu yake anayoipenda zaidi, Arsenal ilipofunga bao.

Bao lililoonekana kumvutia zaidi ni lile la mwisho la mshambulizi Gabriel Jesus katika dakika za mwisho ambalo liliipa Arsenal ushindi wa mabao 3-1.

“Yaaaaay, yaaaay… tatu, mambo ni tatu, mambo ni tatu, mambo ni tatu hapa Emirates.. yaay,” alisikika akishangilia katika video aliyopakia.

Baada ya mechi, alisema kuwa kutazama timu yake anayoipenda zaidi ikiichapa Man United katika uwanja wa Emirates ilikuwa ni hisia nzuri zaidi kuwahi kutokea.

"The Best Experience ever, mabao tatu, pointi tatu, tarehe tatu," alisema.

Aliongeza, “Hisia Bora kabisa. Mancheter United 1, Arsenal 3.. Hisia bora kabisa. Gunners, Arsenali. Mambo ni matatu."

Wanabunduki waliwashinda Mashetani Wekundu 3-1 wakiwa nyumbani na kupata ushindi wao wa tatu katika msimu wa 2023/24 wa Ligi Kuu ya Uingereza. Ushindi huo uliwasogeza hadi nambari 5 kwenye jedwali la EPL wakiwa na alama 10 na tofauti ya mabao manne.

Marcus Rashford wa Manchester United alifungua ukurasa wa mabao katika dakika ya 27 kabla ya nahodha wa Arsenal Martin Odegaard kuwasawazishia dakika moja baadaye. Dakika 90 za kawaida ziliisha kwa sare ya 1-1 lakini wanabunduki waliamka katika dakika za nyongeza na kufunga mabao mawili.

Mchezaji aliyesajiliwa na Arsenal kwa pesa nyingi zaidi, Declan Rice na mshambuliaji Gabriel Jesus walifunga dakika chache kabla ya kipenga cha mwisho kupulizwa, na kuzua shangwe kwenye mamilioni ya mashabiki wa Arsenal kote ulimwenguni.