Kenya sio maskini kwa sababu wanaume wanapenda wanaume!- Boniface Mwangi akosoa vita dhidi ya LGBTQ

Mwangi amekosoa vita dhidi ya ushoga nchini Kenya akisema kuwa tabia hiyo sio tatizo kubwa linaloikabili nchi.

Muhtasari

•Mwangi alibainisha kuwa matatizo yanayoikumba nchi hayachangiwi na suala la watu ambao Wakenya wanaamua kuchumbiana nao.

•Mwangi aliwahimiza watu kufurahia maisha yao jinsi watakavyo bila kujali viwango vya maadili vilivyowekwa nchini, akitaja kuwa hakuna hakikisho la mbinguni kuwepo.

Boniface Mwangi
Boniface Mwangi
Image: HISANI

Mwanaharakati maarufu wa kisiasa na haki za binadamu Boniface Mwangi amekosoa vita dhidi ya ushoga nchini Kenya akisema kuwa tabia hiyo sio tatizo kubwa linaloikabili nchi.

Katika taarifa ndefu kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, baba huyo wa watoto watatu alibainisha kuwa matatizo yanayoikumba nchi hayachangiwi na suala la watu ambao Wakenya wanaamua kuchumbiana nao.

"Ninaishi maisha yangu bila kuomba msamaha. Nitamtetea mtu mzima yeyote ambaye anataka kuishi maisha yake mwenyewe. Viongozi wenu feki wa Kikristo na Kiislamu watakuambia kuwa LGBQTI ndio shida yetu kubwa, sivyo. Kenya sio maskini kwa sababu wanaume wanachumbiana na wanaume, na wanawake wanachumbiana. Kenya ni maskini kwa sababu viongozi wenu wa kidini wanaiba ushuru wetu,” Boniface Mwangi alisema Jumapili asubuhi.

Mwangi alitoa hisia hizo alipokuwa akimjibu Mbunge wa Nyali Mohammed Ali ambaye amekuwa na vita kali naye mtandaoni saa kadhaa zilizopita tangu mwanasiasa huyo kumkosoa kwa kupigania haki za wapenzi wa jinsia moja

Mwangi ambaye kwa sasa yuko likizoni Dubai na mkewe aliendelea kuwahimiza watu kufurahia maisha yao jinsi watakavyo bila kujali viwango vya maadili vilivyowekwa nchini, akitaja kuwa hakuna hakikisho la mbinguni kuwepo.

"Mbingu ni hapa watu. Hakuna aliyekufa, akaenda mbinguni na akarudi na uthibitisho kwamba mitaa ya dhahabu, ambapo watu hunywa maziwa na asali ni kweli. Hata hao mabikira 72 ni hadithi tu. Au labda wale mabikira 72 ni mabikira wa kiume na wewe ni bibi harusi? Acha kuahirisha furaha yako kwa tarehe ya baadaye. Ishi sasa hivi. Upendo sasa hivi. Oa, na umpende unayemtaka,” alisema.

Mwanaharakati huyo aliwataka Wakenya kutojali masuala ya vyumba vya kulala vya watu wengine akitaja kuwa tatizo kuu linalokabili nchi sio kile ambacho watu hufanya katika vyumba vyao vya kulala bali matatizo huanza na viongozi wasio na maadili waliopewa jukumu la kuongoza.

"Ikiwa viongozi wetu wangeweza kufurahia maisha yao ya uasherati hadharani, labda labda tu hawangeiba kama wanavyofanya. Nchi ambazo Ruto HUenda kuomba mikopo hazina sheria sifuri kuhusu maadili lakini zinawafunga wale wafisadi na kuiba. Ondoeni mapua yenu kwenye vyumba vya kulala vya watu," alisema.