Rayvanny hatimaye afichua sababu halisi ya kuondoka WCB, jinsi Diamond alivyoichukulia

Alisema Diamond alimtaka alipe zaidi ya mara dufu ya kiasi ambacho Harmonize alilipa ili kuondoka.

Muhtasari

•Rayvanny ameeleza alihisi amelelewa kimuziki vya kutosha na WCB na ndio maana akapiga hatua kubwa ya kuondoka katika lebo hiyo.

•Alifichua kuwa tayari amekamilisha kulipa kiasi kikubwa cha fedha alichodai Diamond kwa ajili ya kuondoka kwake WCB.

CEO wa Next Level Music
Rayvanny CEO wa Next Level Music
Image: Facebook

Bosi wa lebo ya Next Level Music, Raymond Mwakyusa almaarufu Rayvanny ameeleza kuwa alihisi amelelewa kimuziki vya kutosha na WCB na ndio maana akapiga hatua kubwa ya kuondoka katika lebo hiyo inayomilikiwa na Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na kituo kimoja cha redio cha humu nchini, Rayvanny pia alibainisha kuwa alihisi amekua vya kutosha pia kusaidia wasanii wengine chipukizi.

“Ni hatua tu za kukua za kusonga kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Kwa hiyo nikasema sawa, kwa hatua niliyofika naweza nikasonga mwenyewe na mimi nikashika mkono watu wengine sio tena kushikwa mkono kwa wazazi wanakulea alafu ukikua unatoka,” Rayvanny alisema.

Mwimbaji huyo wa kibao ‘Nitongoze’ alifichua kuwa amefanikiwa kupiga hatua za kujivunia na lebo yake ya NLM tangu alipokuwa msanii wa kujitegemea mwaka jana.

“Wasafi ni familia lakini na pia niko na hatua zangu na nashukuru Mungu. Ni mwaka sasa umepita na naendelea vizuri. Vitu vimekaa vizuri kabisa,” alisema.

Wakati akizungumzia kuhusu kuondoka kwake kwenye lebo ya Diamond, alifichua kuwa alimfahamisha bosi huyo wake wa zamani kuhusu uamuzi wake katika mazingira yasiyo rasmi kisha akajulisha timu nyingine ya WCB.

Aidha, alifichua kuwa kulikuwa na mvutano kuhusu uamuzi wake kabla ya kufikia uamuzi mzuri na kukubaliana kwa njia ya amani.

“Kwanza tulikuwa tu kwenye stori tu za kawaida tukiwa pale kwake alafu nikamgusia kwa sababu namjua. He is proud of me lakini kuna namna mtu anakuwa.. Baadaye alielewa na hakuweka vikwazo vingi. Nilipomwambia alielewa na akaambia timu,” Rayvanny alisema.

Aliongeza “Hata kama kulikuwa na mivutano na nini na nini, lakini tuliweza kumaliza na tukawa na mahusiano mazuri bado. Ni mambo ya riziki, ni mambo ya hela. Kufika kwenye makubaliano sio rahisi. Lakini tuliweza kumaliza kwa njia chanya. Lakini nilimwambia kwa njia isiyo rasmi. Tulikuwa tumekaa tu sebuleni nikamwambia.”

Wakati huo huo, alifichua kuwa tayari amekamilisha kulipa kiasi kikubwa cha fedha alichodai Diamond kwa ajili ya kuondoka kwake WCB.

Bosi huyo wa NLM alidai kuwa kiasi alichodaiwa ni zaidi ya mara mbili ya kiasi ambacho mwimbaji mwenzake, Harmonize alitakiwa kulipa lebo hiyo kufuatia kuondoka kwake miaka kadhaa kabla yake.

“Sio vizuri kusema lakini inaweza kuwa ni mara dufu ya Harmonize. Nililipa. Nimeshalipa. Ni mara dufu na inaongezeka tena kidogo,” alisema.

Kuhusu jinsi alivyojisikia kutakiwa kulipa kiasi kikubwa cha fedha ili aachiliwe, alisema, “Amani ni muhimu zaidi kuliko hizo pesa. Kikubwa ni kuweka ile heshima na kuwa na upendo. Tulimaliza kama familia.”