Mtoto halisi aliyerekodiwa akivuka ‘daraja la mauti’ aibuka baada ya Eric Omondi kupotoshwa (+video)

Erico amesema kuwa bado atasaidia kujenga daraja alilokuwa ameonyeshwa hapo awali pamoja na lile halisi.

Muhtasari

•Eric Omondi alionyeshwa mtoto halisi na daraja halisi ambalo alirekodiwa akivuka baada ya kuelekezwa vibaya mapema Jumanne.

•Mzazi wa mtoto huyo alifichua kuwa watoto wengi huvuka na watu wazima huvuka daraja kila siku wakielekea sehemu zingine.

akivuka daraja hatari
Mtoto akivuka daraja hatari
Image: HISANI

Msichana mdogo wa shule ambaye hivi majuzi alirekodiwa akivuka daraja jembamba hatari juu ya mto uliofurika hatimaye ametambuliwa.

Mchekeshaji Eric Omondi mnamo Jumatano asubuhi alionyeshwa mtoto halisi na daraja halisi ambalo alirekodiwa akivuka baada ya kuelekezwa vibaya mapema Jumanne. Awali alikuwa amepelekwa kwenye daraja lingine hatari katika Kijiji cha Nyakumbati, kaunti ya Kisii lakini baadaye alifahamishwa kuwa halikuwa daraja halisi katika video iliyovuma kwenye mitandao ya kijamii wiki jana.

Siku ya Jumatano asubuhi, mchekeshaji huyo alishiriki video yake akiwa kwenye daraja halisi ambayo alinuia kusaidia katika kuijenga upya na akafunguka kuhusu mambo ya kukatisha tamaa aliyoyaona hapo.

"Leo nilishuhudia mama akiwa amembeba mtoto wake wa miezi 3 akivuka "Daraja la Kifo", niliona watoto wa umri wa mwaka 1 na nusu wakivuka mtego huu wa kifo. Wanawake wakibeba mitungi huku wakichunga maisha yao wenyewe,” Eric Omondi alisema chini ya video aliyoshiriki kwenye Instagram.

Licha ya kupotoshwa hapo awali, Eric alisema kuwa bado atasaidia kujenga daraja alilokuwa ameonyeshwa hapo awali pamoja na lile halisi.

"Tulipata Daraja halisi lakini pia tutajenga Daraja hilo lingine pia kwa sababu wao pia wanalihitaji," alisema.

Kupatikana kwa daraja hilo halisi kumekuja baada ya mwanahabari wa mtandaoni kufanya mahojiano na mzazi wa mtoto halisi aliyerekodiwa akivuka daraja hilo hatari.

“Mahali Eric Omondi ameenda, huyo mtoto anaitwa Shirleen sio huyo. Huyu mtoto wangu anaitwa Ann Kemunto Ondavu. Na mimi naitwa Thomas Ondavu Obure. Yule mtoto ndiye huyu,” baba wa mtoto halisi alisema kwenye mahojiano.

Alifichua kuwa watoto wengi huvuka na watu wazima huvuka daraja kila siku wakielekea shuleni, kanisani na sehemu zingine muhimu.

Katika mahojiano hayo, Bw Ondavu alimtaka mchekeshaji huyo kuwasaidia pia kujenga daraja jipya hata anapojenga lingine katika kijiji cha Nyakumbati.

Jumanne, Eric alijitolea kusaidia jamii ya Kijiji cha Nyakumbati katika Kaunti ya Kisii kujenga daraja mpya baada ya kuonyeshwa ambayo ilidaiwa kuwa daraja kwenye video.

Katika chapisho lake, mchekeshaji huyo alisema alikutana na msichana aliye kwenye video hiyo ambaye alidai anaitwa Shirleen, babake Fred Ogata Mogire, na wanakijiji wengine ambao alizungumza nao kuhusu hali ya daraja hilo.

“Video ya kuhuzunisha ya msichana akivuka Daraja la mauti kwa ujasiri inatoka katika Kijiji cha Nyakumbati katika Kaunti ya Kisii. Msichana anaitwa Shirleen na Baba anaitwa Fred Ogata Mogire,” Eric Omondi alisema.

Aliongeza, ”Jamii hadi sasa imejaribu Kuimarisha Daraja lakini haitoshi. Mbao Imeoza, Inatetemeka na HAIko SALAMA. Ni suala la muda tu kabla ya kuanguka kwenye MSIBA. "

Aliendelea kutangaza kuwa angefanya uchangishaji ili kupata pesa za ujenzi wa daraja hilo.

“Anza Kutuma chochote unachoweza kwa Baba yake Shirleen kwa 0722115399 (JINA: FRED OGATA MOGIRE). TEAM SISI KWA SISI TUJENGE HII LEO, LETS GO!!!,” alisema.