Maelezo mapya kuhusu Bahati yaibuka akikutana na 'kakake' aliyekua naye kwenye Makao ya Watoto

Wawili hao walionekana kujawa na bashasha sana kukutana baada ya miaka mingi.

Muhtasari

•Bahati alifurahi sana kukutana na mmoja wa watu ambao alikua nao katika nyumba ya watoto ya ABC miaka kadhaa iliyopita.

•Bw Nyariro kwa upande wake alisherehekea mafanikio makubwa ya Bahati akifichua kwamba walikuwa wakimwita PHAT. 

alikutana na mwenzake wa zamani katika children's home
Bahati alikutana na mwenzake wa zamani katika children's home
Image: INSTAGRAM// BAHATI

Mwimbaji Kelvin Kioko almaarufu Bahati alifurahi sana kukutana na mmoja wa watu ambao alikua nao katika nyumba ya watoto ya ABC miaka kadhaa iliyopita.

Mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili alichapisha video nzuri ya mkutano wake na mwanamume huyo  aliyejitambulisha kama Francis Nyariro almaarufu ‘Master Lead’ ambaye alithibitisha kuwa walikuwa pamoja nyumbani ya watoto hana hata walizoea kuimba pamoja katika bendi waliyokuwa wameanzisha.

Wawili hao ambao walionekana kufurahi sana kukutana baada ya miaka mingi walikuwa na wakati mzuri sana huku wakishirikishana baadhi ya kumbukumbu kutoka mahali walipoita nyumbani.

"Tulikuwa pamoja na kijana huyu kwenye nyumba ya watoto. Na ndiye pekee aliyeweza kuzungumza Kiingereza kizuri,” Bahati alisema kuhusu rafiki yake.

Aliendelea kueleza jinsi alivyom’miss jamaa huyo aliyekuwa mwenzake katika bendi ya muziki ya KQ Gospel Artisans.

Bw Nyariro kwa upande wake alisherehekea mafanikio makubwa ya Bahati akifichua kwamba walikuwa wakimwita PHAT. (Preaching Holiness And Truth).

"Pia tulizoea kumwita Michael Jackson wa pili," Bw Nyariro alifichua.

Bahati alisema kukutana na rafiki yake huyo kulirudisha kumbukumbu nyingi na kuujaza moyo wake furaha na kicheko.

Mwanamuziki huyo mashuhuri alimpoteza mama yake mzazi akiwa na umri mdogo wa miaka saba. Baada ya mama yake kufariki, mwanamuziki huyo alichukuliwa na ABC Children's Home ambako alilelewa.

Takriban miaka miwili iliyopita, Bahati alifunguka kuwa mama yake alifariki mnamo siku ya Krismasi ndani ya nyumba  akisubiri zamu yake ya kuhudumiwa hospitalini. Wakati huo Bahati alikuwa na umri wa miaka sita.

"Kulikuwa na hospitali moja tu ndogo katika eneo la Mathare. Wiki ambayo mamangu alifariki, hata mimi niliwahi kuamka na mtu saa tisa usiku ili tukampangie foleni hospitalini. Hivyo ndivyo mamangu alivyofariki. Mama yangu alikufa wakati mtu mwingine akiwa  amempigia foleni hospitalini," Bahati alisimulia akiwa kwenye mazungumzo na mkewe Diana Marua.

"Alifariki mida ya adhuhuri. Akakaa kwa nyumba kwa masaa kadhaa. Alasiri ilipofika mwili wake ulikuwa umefungwa kwenye blanketi, tukakodishwa teksi ili tumpeleke mochari" Aliendelea.

Bahati alieleza kuwa hatua ya kumpoteza mamake ilikuwa pigo kubwa kwake na ilimbadilishia maisha sana.

"Nilidhani maisha yangu Nairobi yameisha. Nilijua baada ya maziishi ningepelekwa kuishi Ukambani. Huo ndio ulikuwa mpango. Tulikuwa maskini. Baba yangu hangeweza kumudu sisi kuwa na kijakazI... Nilidhani maisha yangu yameisha. Baada ya mazishi nililia sana ili nisiachwe. Nilijificha kwenye gari iliyokuwa imebeba mwili.Nilianza kuishi na jirani," Bahati alisema.

Baadae, mwanamuziki huyo alienda kuishi kwenye Children's Home hadi alipotimiza umri wa kujisimamia.