"Uchungu usiovumilika na kuchanganyikiwa!" Nazizi afunguka anavyomkosa mwanawe aliyefariki Krismasi

“Nimeku’miss Jazzy wangu, mama anakuhitaji,” Nazizi alizidi kuomboleza.

Muhtasari

•Nazizi ameendelea kumuomboleza marehemu mwanae Jazeel Adam ambaye aliaga dunia takriban miezi mitatu iliyopita.

•Aliendelea kufunguka kuhusu jinsi anavyomkosa sana aliyekuwa mtoto wake wa pili.

Image: INSTAGRAM// NAZIZI

Rapa mkongwe wa Kenya Nazizi Hirji ameendelea kumuomboleza marehemu mwanae Jazeel Adam ambaye aliaga dunia takriban miezi mitatu iliyopita.

Mvulana huyo mwenye umri wa miaka mitatu alikufa mnamo Desemba 25, 2023 kufuatia ajali mbaya iliyotokea katika hoteli moja nchini Tanzania ambako familia ya Nazizi ilikuwa ikikaa. Mwili wa mvulana huyo baadaye ulisafirishwa hadi nchiniKenya baadaye ambako alizikwa mnamo Desemba 26, 2023

Katika taarifa fupi kwenye ukurasa wake wa Instagram, msanii huyo wa dancehall alifichua kwamba hajakuwa sawa kisaikolojia tangu tukio hilo la bahati mbaya.

"Kuzidiwa, kuzama, maumivu yasiyovumilika na kuchanganyikiwa!!," Nazizi alisema kupitia Instastories yake siku ya Jumatano.

Aliendelea kufunguka kuhusu jinsi anavyomkosa sana aliyekuwa mtoto wake wa pili.

“Nimeku’miss Jazzy wangu, mama anakuhitaji,” alisema.

Katikati mwa mwezi uliopita, rapa huyo wa kundi la Neceessary Noize alizungumza kwa hisia kuhusu kifo cha mwanawe huyo aliyeaga na miaka mitatu.

Katika taarifa iliyojaa hisia kali kwenye Instagram, mwimbaji huyo alikiri kwamba haendelei vizuri baada ya kifo cha mwanawe na kushangaa jinsi maisha yake yatakuwa bila mvulana huyo mdogo ambaye alimthamini sana.

"Nimevunjika, nimezama gizani, sitakuwa sawa tena. Je, nitaendeleaje bila nuru ya maisha yangu? Kwa nini niamke kila asubuhi, ili tu kulia na kuku’miss siku nzima? Ulitupenda sana, na tulikupenda hata zaidi, jazzy wangu wa thamani,” Nazizi aliomboleza Jumapili jioni.

Mwimbaji huyo mzaliwa wa pwani aliambatanisha taarifa yake na video iliyoonyesha kumbukumbu nzuri ambayo familia ilishiriki na marehemu Jazeel.

Alibainisha kuwa marehemu Jazeel alileta furaha kubwa kwa familia na akafichua kuwa nia kuu ya mwanawe ilikuwa ni kwamba wote wawe pamoja.

"Video hii inanasa roho yako katika sekunde chache. Ulichowahi kuhitaji ni sisi 4 kuwa pamoja kila wakati. Ulileta maana mpya kwa familia,” aliandika.

Nazizi aliendelea kuzungumzia jinsi maisha yamekuwa katika takriban siku hamsini zilizopita tangu mtoto huyo wake wa miaka mitatu kupoteza maisha kwa bahati mbaya.

“Kijana wangu, maisha hayavumiliki bila wewe 💔💔. Mama anakupenda sana, na ningefanya chochote ili kuwa nawe tena. Sitawahi kuwa sawa, ulimwengu wangu ulisimama uliponiacha jiji. I miss you my sweet boy special,” Nazizi alisema.