Nazizi awajibu wanaomsihi aache kujifungia nyumbani miezi mitatu baada ya kifo cha mwanawe

Awali, mwimbaji huyo aliweka chapisho la kutia wasiwasi wakati akiendelea kuomboleza mwanawe.

Muhtasari

•Nazizi amedokeza kuwa ametumia takriban miezi miwili na nusu iliyopita akiwa amejifungia ndani ya nyumba kufuatia kifo cha mwanawe.

•Aliashiria kuwa wakati mwingine anahisi huzuni sana kuondoka nyumbani na nyakati nyingine anahisi kuondoka nyumbani kunaweza kupunguza huzuni yake.

amemkumbuka kihisia mwanawe
Nazizi amemkumbuka kihisia mwanawe
Image: INSTAGRAM// JAZEEL ADAM

Rapa mkongwe wa Kenya Nazizi Hirji amedokeza kuwa ametumia takriban miezi miwili na nusu iliyopita akiwa amejifungia ndani ya nyumba yake kufuatia kifo cha mwanawe.

Mtoto wa miaka mitatu wa mwimbaji huyo, Jazeel Adam, alipoteza maisha yake mnamo Desemba 25 mwaka jana, kufuatia ajali mbaya iliyotokea katika hoteli ya Tanzania.

Katika taarifa yake siku ya Jumatatu, msanii wa kundi la Necessary Noize aliwashukuru wale ambao wamekuwa wakimtia moyo kuondoka nyumbani na kuungana tena na ulimwengu lakini akadokeza kuwa haijakuwa rahisi kwake tangu mwisho wa mwaka jana.

"Kwa kila mtu anayenitia moyo nitoke nyumbani.. asante lakini, imepita miezi 2 na nusu ya vita hivi..," Nazizi aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuambatanisha ujumbe wake na meme inayoelezea jinsi wakati mwingine anahisi huzuni sana kuondoka nyumbani na nyakati nyingine anahisi kuondoka nyumbani kunaweza kupunguza huzuni yake.

"Vita kwenye ubongo.. Kuhisi huzuni sana kuondoka nyumbani ... Kujua kwamba kwenda nje kutafanya nihisi huzuni imeshuka chini," meme aliyoposti ilisema.

Siku chache zilizopita, mwimbaji huyo aliweka chapisho la kutia wasiwasi wakati akiendelea kuomboleza mwanawe aliyeaga siku ya Krismasi.

"Kwa sababu za kibinafsi, nitakuwa naomboleza leo, kwa sababu watu ninaowapenda waliokufa bado wamekufa sana," posti aliyoweka ilisomeka.

Mtoto Jazeel Adam alikufa mnamo Desemba 25, 2023 kufuatia ajali mbaya iliyotokea katika hoteli moja nchini Tanzania ambako familia ya Nazizi ilikuwa ikikaa. Mwili wa mvulana huyo wa miaka mitatu baadaye ulisafirishwa hadi nchiniKenya baadaye ambako alizikwa mnamo Desemba 26, 2023

Wiki iliyopita, msanii huyo wa dancehall katika taarifa alifichua kwamba hajakuwa sawa kisaikolojia tangu tukio hilo la bahati mbaya.

"Kuzidiwa, kuzama, maumivu yasiyovumilika na kuchanganyikiwa!!," Nazizi alisema kupitia Instastories yake siku ya Jumatano.

Aliendelea kufunguka kuhusu jinsi anavyomkosa sana aliyekuwa mtoto wake wa pili.

“Nimeku’miss Jazzy wangu, mama anakuhitaji,” alisema.