Mwimbaji Nyota Ndogo azungumzia mipango ya kununua ndege ndogo ya kibinafsi

Mwimbaji huyo mzaliwa wa Pwani amedai kuwa ndege anayonuia kununua itafanyiwa majaribio hivi karibuni.

Muhtasari

•Mwimbaji mkongwe Mwanaisha Abdalla almaarufu Nyota Ndogo amedokeza kuhusu mpango wake wa kununua ndege ndogo.

•Alidokeza kuwa ndege anayonuia kununua itamwezesha kukutana na mashabiki wake kutoka maeneo tofauti nchini.

Nyota Ndogo na mume wake Henning Neilsen
Image: INSTAGRAM// NYOTA NDOGO

Mwimbaji mkongwe mzaliwa wa pwani Mwanaisha Abdalla almaarufu Nyota Ndogo amedokeza kuhusu mpango wake wa kununua ndege ndogo.

Katika taarifa yake ya Jumapili jioni, mama huyo wa watoto watatu alidai kuwa ndege anayonuia kununua itafanyiwa majaribio hivi karibuni.

“Kuna ndege nataka kununua lakini mwezi ujao tunafanya kama inaweza kupaa kutoka Voi hadi Diani,” Nyota Ndogo alisema kupitia Instagram.

Aliambatanisha taarifa yake na picha ya ndege ndogo ambayo sanasana hutumiwa zaidi kwa safari za ndani.

Mwimbaji huyo alidokeza kuwa ndege anayonuia kununua itamwezesha kukutana na mashabiki wake kutoka maeneo tofauti nchini.

“Nafikiri nitakuwa na uwezo wa kuwatembelea hata mashabiki zangu. Kadogo tu kakuweza kuingia hata mitaani. Hebu semeni Amin,” alisema.

Haijabainika iwapo mwanamuziki huyo mkongwe ambaye sasa anaendesha hoteli katika eneo la Voi ana nia ya kutaka kununua ndege au ni ndoto tu.

Haya yanajrii siku chache tu baada ya mwanamuziki huyo kulazimika kujitetea vikali baada ya kushtumiwa kwa kupokea chakula kutoka kwa gavana wa zamani wa Mombasa, Ali Hassan Joho.

Nyota Ndogo alikuwa miongoni mwa Waislamu waliopokea chakula kilichokuwa kikisambazwa na Joho katika kaunti ya Taita Taveta, na hilo liliwavutia wengi kumshtumu kwamba hakustahili kupokea cakula hicho kwani kilikusudiwa kwa watu wasiojiweza wakati wa mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadani.

Hata hivyo, katika mahojiano kwa njia ya simu kupitia kituo kimoja cha redio humu nchini, Nyota Ndogo alisema kwamba asingekataa kupokea chakula hicho kwani hakikusudiwa kuwa msaada kwa maskini bali kilikuwa ni chakula kwa Waislamu wote waliofunga.

“Chakula kilikuwa kwa sababu ya mfungo wa Ramadan, hakikuwa chakula cha misaada, hakikuwa chakula cha kupatia wasiojiweza. Joho aliona wacha nipeane futar kwa ajili ya Ramadan, watu waliofunga sio watu wasiojiweza,” alifafanua Nyota Ndogo.

Akifafanua kuhusu kuitwa tajiri ambaye hastahili kupokea chakula, Nyota Ndogo alisema kwamba ni umbea na roho mbaya tu na kusema kwamba hakuna hata siku moja anakumbuka aliwahi jitangaza kuwa yeye ni tajiri.

“Watu waache roho mbaya na hakuna siku nishawahi jitangaza kwamba mimi ni tajiri, ama niko na pesa. Ningekuwa nina pesa ningepika chapatti pale siku mzima,” alisema