Akothee asherehekea mafanikio makubwa licha ya matatizo ya mahusiano na malezi

Katika taarifa yake, Akothee alibainisha kuwa amepitia matatizo mengi, lakini hilo halijamzuia kujizolea mafanikio.

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo alitumia siku hiyo kusherehekea mafanikio yake makubwa maishani hadi sasa na pia kuwatia moyo watu wengine.

Licha ya kulea watoto katika familia zilizovunjika, kuvumilia mahusiano yaliyofeli, na kuendesha biashara zilizofanikiwa, sikukata tamaa,” Akothee alisema

Eshter Akothee/Instagram
Eshter Akothee/Instagram
Image: HISANI

Mwanamuziki na mjasiriamali mashuhuri wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee, mnamo Jumatano, aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa ya 43 kwa njia maalum.

Mama huyo wa watoto watano alitumia siku hiyo kusherehekea mafanikio yake makubwa maishani hadi sasa na pia kuwatia moyo watu wengine.

Katika taarifa yake kwenye mtandao wa Instagram, alibainisha kuwa amepitia matatizo mengi, lakini hilo halijamzuia kujizolea mafanikio.

"Kushindwa mara elfu kulinifunza njia elfu moja ambazo hazikufanya kazi. Maisha yamejaa changamoto, lakini mafanikio huja kwa kuendelea kujifunza na kukua.

Licha ya kulea watoto katika familia zilizovunjika, kuvumilia mahusiano yaliyofeli, na kuendesha biashara zilizofanikiwa, sikukata tamaa,” Akothee alisema.

Aliongeza, "Nilifanikiwa kuhitimu shahada yangu nikiwa na miaka 42 na kuwa mkurugenzi wa shule yenye wanafunzi 70 na walimu 18 nikiwa na miaka 42.  Siadhimishi siku yangu ya kuzaliwa, nahesabu mafanikio yangu katika miaka niliyoishi."

Pia alizungumza kuhusu ujasiri wake na kuweka wazi kwamba hawezi kushushwa.

"Huna haja ya kunikumbusha kufeli kwangu, niko bize nahesabu mafanikio yangu, usiniambie mimi ni nani, hunijui. Najijua vizuri sana.

MIMI NI MWANAMKE MWENYE UJASIRI WA AJABU Furaha ya Siku ya Kuzaliwa kwa Malkia wa "NITACHUKUA KICHWA NA NITAISHUGHULIKIA," alisema.

Mwishoni mwa mwaka jana, Akothee aliipongeza kwa kufaulu kumaliza kozi yake ya digrii baada ya miaka kumi na minne ya masomo.

Mwanamuziki huyo alihitimu rasmi na Shahada ya Kwanza ya Usimamizi wa Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Mt Kenya mnamo Desemba. Alisherehekea mafanikio hayo na kuyataja kama dhihirisho la ukakamavu usioyumbayumba.

Akothee alianza kozi yake ya shahada katika chuo kikuu hicho cha kibinafsi zaidi ya mwongo mmoja uliopita na ni miongoni mwa maelfu ya wahitimu ambao watapokea taji lao mwaka huu.

“Leo (Desemba 8), tunashuhudia ushindi wa miaka 14 tangu... Kuhitimu kwa ESTHER AKOTH KOKEYO kutoka chuo kikuu cha MT KENYA darasa la BBM la 2023 sio tu mafanikio ya kitaaluma; ni dhihirisho la ustahimilivu usioyumba,” Akothee alisema Desemba  mwaka jana.

Aliongeza, “Katika kukabiliana na dhiki, safari ya Akothee inaashiria roho ya mwanadamu isiyoweza kushindwa. Kuhitimu kwake sio tu ushindi wa kibinafsi lakini msukumo kwa wote wanaothubutu kuota dhidi ya uwezekano wowote.

Hongera, ESTHER AKOTH KOKEYO AKOTHEE, kwa mafanikio haya ya ajabu💪 Uthabiti wako ni mwanga, unaoangazia njia kwa wale wanaoamini katika nguvu ya mabadiliko ya elimu. Hongera kwa safari iliyosafirishwa vyema na siku zijazo zilizojaa uwezekano usio na kikomo. Hongera sana MIN OYOO.”