Huzuni Nigeria huku Muigizaji mwingine wa Nollywood, Zulu Adigwe akiaga dunia

Tasnia ya filamu ya Nigeria inaomboleza tena kufuatia kifo cha migizaji mwingine mkongwe, Zulu Adigwe.

Muhtasari

•Kifo cha Zulu Adigwe kilithibitishwa na mtayarishaji wa filamu, Stanley Nwoko, kupitia  ukurasa wake wa Instagram.

Marehemu Zulu Adigwe
Image: HISANI

Tasnia ya filamu ya Nigeria inaomboleza tena kufuatia taarifa za kifo cha migizaji mwingine mkongwe wa Nollywood, Zulu Adigwe aliyefariki Jumanne jioni.

Kifo cha muigizaji huyo mkongwe kilithibitishwa na mtayarishaji wa filamu, Stanley Nwoko, kupitia chapisho kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Hata hivyo hakueleza sababu ya kifo chake.

“Nasikitika kutangaza kuaga kwa muigizaji mkongwe, marehemu Bw Zulu Adigwe. Kilichosababisha kifo chake bado hakijaangaliwa. Pumzika kwa amani muigizaji mzuri,” Nwoko alisema.

Marehemu aliigiza filamu za Isakaba, Unforgettable, Blood Diamond, The Powerful Baby, Grandmaster, My Promise, City of Kings, Divided Heart, na nyinginezo nyingi. Aliigiza sana kama chifu, mtawala wa kitamaduni, baba, au mzee.

Kifo cha Zulu kimekuja mwezi mmoja tu baada ya muigizaji mwenzake mkongwe wa Nollywood Amaechi Muonagor pia kufariki.

Bw Muonagor alithibitishwa kufariki mnamo Machi 24  baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa figo kwa muda mrefu.

Alifariki akiwa na umri wa miaka 62.

Vyombo vya habari vya Nigeria viliripoti kuwa mwigizaji huyo wa vichekesho alikuwa kwenye matibabu ya dialysis kabla ya kifo chake. Alikuwa amepooza kwa sehemu kutokana na ugonjwa wa figo ambao umechukua maisha yake.

Kifo cha muigizaji huyo mkongwe kilikuja siku chache baada ya video kusambaa ambapo alionekana akiomba msaada wa kifedha kutoka kwa Wanigeria ili kumwezesha kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya upandikizaji wa figo.