"Namshukuru Mungu!" Betty Kyallo ajawa bashasha huku akirejea kwenye TV baada ya miaka 4

Haya yanajiri wiki chache tu baada ya saluni yake 'Flair with Betty' kupigwa mnada.

Muhtasari

•Betty alifichua kuwa amejiunga na kampuni ya Cape Media Limited ambako atafanya kazi kama mtangazaji wa TV47.

•Alitangaza kuwa kipindi chake kitaitwa ‘This Friday With Betty’ na akaahidi mambo mengi ya kushangaza kwa watazamaji wake.

Image: INSTAGRAM// BETTY KYALLO

Siku ya Ijumaa jioni, mtangazaji maarufu Betty Mutei Kyallo alitangaza kurejea kwake kwenye TV.

Katika taarifa kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, mama huyo wa binti mmoja alifichua kuwa amejiunga na kampuni ya Cape Media Limited ambako atafanya kazi kama mtangazaji wa TV47.

Betty amekuwa mbali na skrini za TV kwa takriban miaka minne na wakati akitangaza kurudi kwake Ijumaa, alisema anafurahi kukutana na watazamaji wake tena.

"Baada ya karibu miaka minne. Nimerudi. TV47 sasa ni nyumba yangu. Siwezi kusubiri kukuona hadhira yangu nzuri. Hili ni jukwaa langu bora! Yaaaay! Tutaonana hivi karibuni,” Betty Kyallo alitangaza kwenye Instagram.

Mtangazaji huyo mrembo alitangaza kuwa kipindi chake kitaitwa ‘This Friday With Betty’ na akaahidi mambo mengi ya kushangaza kwa watazamaji wake.

Kyallo alianzia kituo cha KTN ambapo alifanya kazi kama mwanafunzi wa ndani kabla ya kuajiriwa kama mtangazaji mkuu wa habari ambapo alipeperusha habari za saa tatu usiku siku ya Ijumaa zilizopewa jina la Friday Briefing.

Baadaye, alijiunga na K24 ambapo alipeperusha kipindi cha wikendi cha 'Up Close with Betty'.

Aliondoka K24 mwishoni mwa Mei, 2020, katikati ya janga la Covid-19 na kuanzisha biashara yake ya saluni na spa katika mtaa wa Kilimani iliyopewa jina la Flair by Betty.

Mwezi uliopita, Kyallo alisema kodi ya nyumba imekuwa mzigo mkubwa kwa biashara yake na kusababisha saluni yake ya Flair by Betty kupigwa mnada kutokana na malimbikizo ya kodi.

“Kuendesha biashara nchini Kenya imekuwa vigumu sana. Wamiliki wa nyumba hawataki kupunguza kodi na inakuwa mzigo mkubwa kwa biashara ambazo zinatatizika kwa sababu ya kudorora kwa uchumi,” Kyalo alisema kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Katika tangazo la umma kwenye magazeti ya kila siku, Keysian Auctioneers walichapisha bidhaa kwenye majengo ambayo yalipaswa kuuzwa kwa mnada wa umma mnamo Aprili 17, 2024.

Bidhaa hizo ni pamoja na rafu tatu za visima vilivyobomolewa, sehemu ya kitanda cha kufanyia masaji, vitanda viwili vya kufanyia masaji, sehemu ndogo ya kuwekea vifaa, rafu ya glasi, vioo vinne vikubwa, viyosha joto vya taulo na meza za kuvaa.

Mamia ya mashabiki sasa wamezamia kwenye mitandao ya kijamii kumkaribisha Betty Kyallo tena kwenye runinga anaporejea kufanya kile anachofanya vyema zaidi.