"Amekuwa nao karibu miaka 18!" Muigizaji Makokha afichua kilichomuua mkewe

Alisema kuwa tayari alikuwa ametumia pesa nyingi kwa matibabu na dawa za mkewe.

Muhtasari

•Muigizaji huyo mcheshi alifichua kuwa marehemu Wambui alipambana na Saratani ya Matiti kwa karibu miongo miwili.

•Makokha alisema alijaribu sana kumsaidia marehemu mke wake kadri ya uwezo wake tangu alipogundulika kuugua ugonjwa huo hatari.

Makokha na marehemu mkewe
Makokha na marehemu mkewe
Image: HISANI

Muigizaji na mcheshi mkongwe wa Kenya Matayo Keya almaarufu Alphonse Makokha Makwacha amefunguka kuhusu ugonjwa ambao marehemu mkewe Purity Wambui alikuwa akiugua.

Katika mazungumzo ya kipekee na Tuko Kenya, muigizaji huyo wa kipindi cha Vioja Mahakamani alifichua kuwa marehemu Wambui alipambana na Saratani ya Matiti kwa karibu miongo miwili.

Alisema ugonjwa huo ulikithiri takriban miezi minne iliyopita ambapo madaktari waliwafichulia kwamba ulikuwa umesambaa sehemu zingine za mwili ikiwemo uti wa mgongo.

"Imekuwa muda mrefu, karibu miezi minne ikienda sana. Nikawa nampeleka hospitali anapona, tena anarudi anakaa kama hajapona..” Makokha alisimulia.

Aliongeza, “Shida ni saratani ya matiti. Aliposhikwa na ile ugonjwa wa saratani ya matiti ndiyo akawa anaenda kufanyiwa chemotherapy. Kuna uvimbe ambazo zilikuwa zinatolewa kwenye matiti. Yeye ni shujaa. Amekuwa na ugonjwa huo kwa karibu miaka 18.”

Muigizaji huyo mcheshi alibainisha kwamba alijaribu sana kumsaidia marehemu mke wake kadri ya uwezo wake tangu alipogundulika kuugua ugonjwa huo hatari.

Alisema kuwa tayari alikuwa ametumia pesa nyingi kwa matibabu na dawa za mkewe, na amekuwa akijaribu kumsaidia peke yake bila kutafuta msaada.

“Imeniathiri kifedha, kisaikolojia pia kwa sababu singeweza kuambia watu kile kinaendelea. Iliniathiri kusema kweli, singeweza kuwa imara. Lakini ukiniona, niko na furaha sana,” alisema.

Makokha alifichua kuwa mkewe alifariki nyumbani akiwa chini ya uangalizi wa binti yao. Yeye alikuwa ameenda kazini alipopata habari hizo za kusikitisha.

“Nilikuwa naenda kazini. Nilikuwa nimewacha binti yangu nikamwambia amuangalie mama yake, naenda kutafuta riziki,” alisimulia.

Alifichua kuwa ni muigizaji mwenzake Hiram Mungai almaarufu Ondiek Nyuka Kwota ambaye alifahamishwa wa mara ya kwanza kuhusu kufariki kwa mkewe.

Ondiek kisha akamjulisha kuhusu habari hizo za kusikitisha kwa njia ya huruma.

“Nililia kwa muda wa saa mbili hivi. Mimi ndiye nilikuwa nikiendesha gari, yeye (Ondiek) alichukua usukani na kuendesha. Nikasema kwa sababu imefanyika, tuendelee na safari. Nikaenda kazini tu kama kawaida. Hiyo siku tulikuwa tulale lakini ata sikulala, lazima ningerudi. Mungu alinipatia nguvu nikawapeleka nyumbani vizuri, pia mimi nikafika nyumbani vizuri,” alisema.

Makokha alisema kuwa baada ya kufika nyumbani jioni hiyo, alikuwa na usiku mbaya kwani alilia sana hadi mida ya asubuhi.

Muigizaji huyo alisema tayari anakosa kelele ambazo mkewe alikuwa akimpigia nyumbani.

Alisema tukio hilo la kusikitisha limeacha jeraha kubwa ambalo hana uhakika kama litapona.

“Inauma, inauma. Ni uchungu kwa sababu sitakuwa tena na jiko yangu karibu ambayo nilikuwa naipenda,” alisema kwa uchungu mwingi.