Mabinti 4 wa mchekeshaji Alphonse Makokha wamuomboleza mama yao kwa jumbe za kihisia

Kila mmoja alikuwa na ujumbe maalum kwa marehemu , akieleza upendo wake kwake na kukiri jinsi wanavyomkumbuka.

Muhtasari

•Katika wasifu wa marehemu ulioifikia Radio Jambo, ilibainika kuwa marehemu alikuwa na binti wanne pamoja na muigizaji Makokha.

•Kila mmoja wao alikuwa na ujumbe maalum kwa marehemu mzazi wao, akieleza upendo wake kwake na kukiri jinsi wanavyomkumbuka.

Makokha na marehemu mkewe
Makokha na marehemu mkewe
Image: HISANI

Maelezo kadhaa kuhusu familia ya muigizaji Matayo Keya almaarufu Alphonse Makokha yameibuka katika wasifu wa marehemu mkewe Purity Wambui.

Marehemu Wambui anazikwa leo, Alhamisi, Juni 13 katika Makaburi ya Lang’ata, Nairobi. Alikufa mnamo Juni 1, 2024 baada ya vita vya muda mrefu na Saratani.

Katika wasifu wa marehemu ulioifikia Radio Jambo, ilibainika kuwa marehemu alikuwa na binti wanne pamoja na muigizaji Makokha.

“Purity alifunga ndoa na Matayo Msagani Keya mwaka wa 1993, na walishiriki miaka mingi ya ajabu. Ndoa yao ilijaa upendo, heshima, na kusaidiana. Walibarikiwa wasichana wanne warembo; Maline, Sharlet, Shanice, na Malia Msagani,” wasifu huo ulisomeka.

Mabinti hao wanne pia walimuomboleza marehemu mama yao katika wasifu huo.

Kila mmoja wao alikuwa na ujumbe maalum kwa marehemu mzazi wao, akieleza upendo wake kwake na kukiri jinsi wanavyomkumbuka.

Maline Msagani: Mama nimeku’miss sana. Asante kwa kuwa daima kwa ajili yetu na kutufundisha kuwa na nguvu. Nakupenda.

Sharlet Msagani: Pumzika kwa amani mummy, ndiyo tunasikitika kwa sababu ulituacha lakini pia tunafurahi kwamba umepumzika na huna maumivu. Nakupenda.

Shanice Msagani: Mama, ulikuwa mwamba wangu. Ulinionyesha maana ya kuwa jasiri, kutokuwa na upuuzi na kuwa mtu wa kwenda kutafuta. Ninaahidi kumtunza baba na Puuh jinsi kama ulivyofanya. Nakupenda daima Wambire.

Malia Msagani: Nime’miss kucheza na wewe. Asante kwa kukumbatiana na hadithi bora. Nakupenda sana na nitakukumbuka daima.

Mke wa Makokha, marehemu Purity Wambui alipoteza maisha mnamo Juni 1, 2024 baada ya kuugua saratani ya matiti kwa muda mrefu.

Katika mahojiano ya hivi majuzi, muigizaji huyo mkongwe alifichua kuwa mkewe alifariki akiwa nyumbani. Alisema kuwa marehemu alikuwa chini ya uangalizi wa binti yao wakati alifariki.

“Nilikuwa naenda kazini. Nilikuwa nimewacha binti yangu nikamwambia amuangalie mama yake, naenda kutafuta riziki,” alisimulia.

Alifichua kuwa ni muigizaji mwenzake Hiram Mungai almaarufu Ondiek Nyuka Kwota ambaye alifahamishwa wa mara ya kwanza kuhusu kufariki kwa mkewe.

Ondiek kisha akamjulisha kuhusu habari hizo za kusikitisha kwa njia ya huruma.

“Nililia kwa muda wa saa mbili hivi. Mimi ndiye nilikuwa nikiendesha gari, yeye (Ondiek) alichukua usukani na kuendesha. Nikasema kwa sababu imefanyika, tuendelee na safari. Nikaenda kazini tu kama kawaida. Hiyo siku tulikuwa tulale lakini ata sikulala, lazima ningerudi. Mungu alinipatia nguvu nikawapeleka nyumbani vizuri, pia mimi nikafika nyumbani vizuri,” alisema.

Makokha alisema kuwa baada ya kufika nyumbani jioni hiyo, alikuwa na usiku mbaya kwani alilia sana hadi mida ya asubuhi.