Azziad avunja kimya baada ya kupata uteuzi wa serikali, aahidi kutekeleza majukumu yake

Mtumbuizaji huyo ameahidi kutumia ujuzi wake wa sanaa kukuza sekta ya ubunifu nchini.

Muhtasari

•Azziad ametoa shukrani za dhati kwa wizara ya Michezo na Sanaa kufuatia uteuzi wake kama mwanachama wa Kamati ya Kiufundi ya Ubunifu.

•Azziad libainisha kwamba yupo tayari kushirikiana na wengine walioteuliwa pamoja na wadau husika kwenye kamati hiyo ili kukuza sekta ya sanaa na ubunifu ya Kenya.

Image: INSTAGRAM// AZZIAD NASENYA

Mtumbuizaji wa Tiktok Azziad Nasenya ametoa shukrani za dhati kwa wizara ya Michezo na Sanaa na Waziri wake Ababu Namwamba kufuatia uteuzi wake kama mwanachama wa Kamati ya Kiufundi ya Ubunifu.

Kulingana na notisi ya gazeti la serikali iliyotolewa Februari 10, waziri Ababu Namwamba alimteua Azziad miongoni mwa watu wengine mashuhuri akiwemo Daniel 'Churchill' Ndambuki,  Jimmi Gathu, Catherine Kamau, Akothee na  Wahu Kagwi kuhudumu kwenye kamati hiyo kwa miaka mitatu.

Azziad sasa ameipokea uteuzi huo kwa mikono miwili na kueleza kuridhishwa kwake na jukumu alilopewa la kuhudumia taifa. Kufuatia hilo, ameahidi kutumia ujuzi wake wa sanaa kukuza sekta ya ubunifu nchini.

"Mimi ni muumini thabiti wa uwezo wa uchumi wa ubunifu kama taaluma inayotimiza na chanzo cha mapato, na mnufaika wa hiyo hiyo. Kwa hivyo ninajitolea kutumia ujuzi na uzoefu wangu niliopata katika  ulimwengu wa dijitali kama mtayarishaji wa maudhui ili kusaidia ukuaji wa sekta ya ubunifu na kuhakikisha kwamba maono ya Talanta Hela yanatimizwa," alisema katika taarifa yake ya Instagram siku ya Jumatatu.

Mtumbuizaji huyo mwenye umri wa miaka 22 alibainisha kwamba yupo tayari kushirikiana na wengine walioteuliwa pamoja na wadau husika kwenye kamati hiyo ili kukuza sekta ya sanaa na ubunifu ya Kenya.

"Ninaamini kuwa kwa sapoti yenu, mustakabali wa uchumi wa ubunifu ni mzuri. Kwa pamoja tuweke pesa mifukoni mwetu," alisema.

Azziad alipata umaarufu mkubwa mnamo Aprili 2020 baada ya kuchapisha video ya dansi ya wimbo wa Femi One na Mejja ‘Utawezana’ ambayo ilisambaa kwenye mitandao yote ya kijamii na kupokelea upendo kutoka kwa wanamitandao wengi. Tangu wakati huo, amepata kazi nyingi katika tasnia ya burudani na uuzaji.