"Wakae chini waelewane" Mzee Abdul amsihi mwanawe Diamond Platnumz amalize ugomvi wake na Harmonize

Muhtasari

•Mzee  Abdul alimsihi Diamond ashiriki kikao na Harmonize wazungumzie tofauti zao na waelewane.

•Mzee Abdul alisema hana kinyongo chochote dhidi ya mwanawe wala mpenzi wake wa zamani, Mama Dangote kwani alishawasamehe na kusahau yaliyopita.

Diamond Platnumz, Mzee Abdul, Harmonize
Diamond Platnumz, Mzee Abdul, Harmonize
Image: HISANI

Baba mzazi ya Diamond Platnumz, Mzee Abdul Juma  ametoa wito kwa mwanawe kuelewana na mwenzake wa zamani Rajab Abdul Kahali almaarufu kama Harmonize.

Alipokuwa kwenye mahojiano na Mbengo TV hivi majuzi, mzee  Abdul alimsihi Diamond ashiriki kikao na Harmonize wazungumzie tofauti zao na waelewane.

Mzee huyo ambaye alitengana na mamake Diamond, Mama Dangote miaka mingi iliyopita ameomba serikali na walio karibu na nyota wale wawili wa Bongo kuwapatanisha kuona kuwa wote wanaipeperusha bendera ya Tanzania.

"Wakae tu waelewane, hii dunia ni mapito basi. Yakitokea maneno kama haya wanaotoa hisia wawaagize waelewane wawe pamoja. Alafu tena waziri wa michezo kama yupo vilevile kuna uwezekano wa kuwaita. Mama Naseeb Sanura na Shamte kama wana uwezo wanaweza wakawaita wakaomgea, wakawaweka chini. Watoto  kama watawasikiliza waongee kama ndugu waelewane"  Alisema Mzee Abdul.

Mzee Abdul alisema hana kinyongo chochote dhidi ya mwanawe wala mpenzi wake wa zamani, Mama Dangote kwani alishawasamehe na kusahau yaliyopita.

Siku kadhaa zilizopita Harmonize alifunguka kuhusu ugomvi wake na aliyekuwa bosi wake katika WCB Diamond Platnumz.

Konde Boy alisema Diamond pamoja na mameneja wake walianza kumuonea gere wakati nyota yake ilianza kung'aa zaidi hadi akatangaza vita dhidi yake.

"Aliniambia eti 'mimi nikimpa mtu heshima yangu, asiponirudishia naichukua kinguvu. Unataka kushindana na mimi na huniwezi kiserikali, huniwezi kihela na huniwezi kiuchawi. Nipe mkono tushindane.' Mimi nilibaki nimeduwa nikajiuliza kama tumefikia hatua hiyo keshoye mtu angeweza kuniwekea sumu nikafa" Alisema Harmonize

Harmonize alisema kabla yake kutoka Wasafi alikuwa amejaribu sana kurejesha uhusiano mzuri na Diamond bila mafanikio.