"Nilihisi kama atakufa!" Sandra Dacha azungumzia ugonjwa uliokuwa umeathiri Akuku Danger hadi akalazwa ICU

Muhtasari

•Dacha alisema mapafu ya mchekeshaji huyo yalikuwa yamejawa na maji na kuathirika sana kiasi cha kwamba madaktari walisema alihitaji maombi mengi ili kutoka hospitali akiwa hai.

•Alisema alilia sana wakati alifika hospitalini na kupata mpenzi wake akiwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwani alikuwa amelemewa sana.

Image: INSTAGRAM// SANDRA DACHA

Mwigizaji mashuhuri Sandra Dacha almaarufu kama Silprosa amefichua kwamba mpenzi wake mchekeshaji Akuku Danger alikuwa amelazwa hospitalini baada ya kushambuliwa na ugonjwa wa Pneumonia.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, Dacha alieleza kwamba ugonjwa huo ulikuwa umeathiri 75% ya mapafu ya Akuku Danger na kumwacha katika hali mahututi.

Dacha alisema mapafu ya mchekeshaji huyo yalikuwa yamejawa na maji na kuathirika sana kiasi cha kwamba madaktari walisema alihitaji maombi mengi ili aweze kutoka hospitali akiwa hai.

"Pneumonia ilikuwa imekula 75% ya mapafu yake, ilikuwa imebaki 25%. Asilimia 75 ni kubwa. Alikuwa na pneumonia na ndio maana alikuwa na matatizo ya kupumua. Madaktari walishinda wakitwambia maombi ni muhimu. Maji ilikuwa imejaa kwa mapafu. Ilikuwa kati yake  na Mungu, ni Mungu" Dacha alisema.

Mwigizaji huyo alisema alifahamishwa kwamba Akuku Danger anaugua mnamo mkesha wa mwaka mpya.

Dacha alisema alilia sana wakati alifika hospitalini na kupata mpenzi wake akiwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwani alikuwa amelemewa sana.

"Ilikuwa mbaya. Nilihisi kama kwamba angekufa. Madaktari walikuwa wanasema tuombe Mungu. Lakini Mungu ni nani, amepona" Dacha alisema.

Dacha amehakikishia mashabiki kwamba afya ya Akuku Danger imeimarika na tayari ameruhusiwa kwenda nyumbani.

Hata hivyo amewasihi kuendelea kuchanga kwani bado hawajakamilisha kulipa bili ya hospitali. Amesema walikubaliana na usimamizi wa hospitali kwamba salio lingelipwa ndani ya kipindi cha wiki tatu.