'Heshimu mke wangu!' DJ Mo afichua sababu zake kumfurusha Ringtone kwenye hafla ya Size 8

Muhtasari

•Mo alimshutumu Apoko kwa kutomheshimu mkewe na kukiuka mipaka yao, jambo ambalo alisema halikumpendeza na hivyo kulazimika kuchukua hatua.

•Alisema kwamba alijaribu kumsihi Apoko ajitoe nje bila mkwaruzano ila akakaidi na kuanzisha vurugu.

Pamoja:Size 8 na DJ Mo

Siku ya Jumapili mwanamuziki wa nyimbo za injili Linet Munyasia almaarufu kama Size 8 alizindua albamu yake ya kwanza.

Wageni kadhaa ikiwemo wanamuziki, wanahabari na marafiki wa karibu walialikwa kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa albamu   'Christ Revealed' ambayo ilifanyika katika hoteli ya Panari, Nairobi.

Moja ya tukio kubwa la kukumbukwa zaidi la siku hiyo lilikuwa mume wa Size 8, DJ Mo kumfukuza mwenyekiti wa wanamuziki wa injili wa kujitangaza Ringtone Apoko. 

Mcheza santuri huyo alimshutumu Apoko kwa kutomheshimu mkewe na kukiuka mipaka yao, jambo ambalo alisema halikumpendeza na hivyo kulazimika kuchukua hatua.

"Kama sisi ni marafiki, acha tuwe marafiki. Nikihisi kama kwamba unaenda kuongea kitu dhidi ya mke wangu, basi unaniguza pabaya. Sisi kama wanaume marafiki lazima tuhakikishe tumelinda watu wetu. Ukija hapa useme eti Size 8 alifanya nini na nini, hiyo si poa" Alisema DJ Mo.

Baba huyo wa watoto wawili pia alimshutumu Apoko kwa kutumia hafla hiyo kubwa kwa mkewe kutafuta kiki.

Mo alidai kwamba isingekuwa ni wokovu wake, basi angechukua hatua baya zaidi dhidi ya mwanamuziki huyo anayejulikana kuzingirwa na drama tele  maishani.

"Huwezi toa watu nje wakati hafla inaendelea uanze kuwaambia ujinga. Ndio maana nilifanya nilichostahili kufanya. Isipokuwa ni wasee wangu walinisimamisha ingekuwa baya zaidi. Ninachosema ni kwamba, popote mimi ama mke wangu alipo, usikuje kutafuta kiki. Tuheshimiane!" Mo alisema.

Mcheza santuri huyo alisema kwamba alijaribu kumsihi Apoko ajitoe nje bila mkwaruzano ila akakaidi na kuanzisha vurugu.