Steven Nyerere atoa tamko lake, "Sing'atuki hata kwa dawa!"

Muhtasari

• Msemaji na bwana mipango mteule katika shirikisho la sanaa nchini Tanzania, Steven Nyerere  ametoa tamko lake kuhusu pingamizi za wasanii kwa uteuzi wake.

• Amesema hana mpango wowote wa kung'atuka licha ya shinikizo na kusema kwamba iwapo watamtengua basi ataelekea mahakamani.

Msemaji na mratibu wa shughuli za sanaa Tanzania, Steven Nyerere
Msemaji na mratibu wa shughuli za sanaa Tanzania, Steven Nyerere
Image: INSTAGRAM

Sakata la uteuzi wa Steven Nyerere kuwa msemaji wa Sanaa ya bongo fleva bado linazidi kukolea zaidi huku wasanii wakigawanyika pakubwa kuhusu uteuzi wake.

Wapo wale wanaoona kwamab uteuzi wake kuwa msemaji na bwana mipango wa shirikisho la Sanaa ni haki na upande wa pili kuna wale wanaosema hakufaa kupewa nafasi kama hiyo kwa sababu yeye si msanii wa muziki.

Baada ya shinikizo kutia mkakasi na joto kupanda, hatimaye msemaji mteule, Steven Nyerere amevunja ukimya wake na kutoa tamko lake kuhusu ishu hiyo ambayo imepata jina lake likitajwa kwa ubaya na uzuri kwa mgao sawa.

Nyerere amesisitiza kwamab ameshateuliwa na kuchukua majukumu yake kama msemaji na mratibu wa mipango ya shughuli za Sanaa na katu hawezi ng’atuka hata kwa dawa.

“Nawaambia tu, sijiuzulu na wala sitoki. Nina nia ya kuendeleza industry ya nchi hii,” alisema Nyerere.

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa wasanii kumtengua katika kikao ambacho wamekiitisha tarehe ishirini na moja, Nyerere alisema kwamba kuna taasisi za mahakama na suala hilo litakaa kisheria zaidi kama wasanii wataamua kuenda katika mkondo huo.

Akijitolea mfano kama Yesu, Nyerere alisema kwamba yeye ni kama mti wenye matunda na haoni vibaya kutupiwa mawe kwani hata Yesu hakuwa anapendwa na kila mtu hata baada ya kufanya kazi kubwa ya kuponya watu wenye matatizo mbalimbali, mwisho wa siku alipigwa misumari kwenye msalaba.