"Wakigusa bei ya tissue nabadilisha dini!" Inspector Mwala atishia

Muhtasari

• Mchekeshaji Inspector Mwala ametishia kubadilisha dini kwenda Uislam iwapo bei ya tissue itapanda.

• Ikumbukwe ipo dhana kwamba Waislam huwa wanatumia maji kama mbadala ya kopo la msalani katika haja kubwa.

Mchekeshaji Inspekta Mwala
Mchekeshaji Inspekta Mwala
Image: Facebook

Hali ya uchumi inazidi kuchukua mkondo wa hekaya za Afadhali ya jana kila kuchao nchini kenya huku idadi kubwa na wananchi wa maisha ya chini wakishindwa kujikimu kimaisha, achia mbali kumudu milo mitatu kwa kila siku iendayo kwa Mungu.

Hali hii mbaya inazidi kuwasakama Wakenya wote si matajiri si maskini kwani wote kwa njia moja au nyingine wamejipata wakigugunwa na hatari hii, na sasa baadhi ya Wakenya wamejitokeza katika mitandao ya kijamii kulalamika huku wengine wakitolea mifano ya bei za bidhaa ambazo zikiathirika tu watafanya maamuzi ya kushangaza taifa zima.

Mchekeshaji mkongwe Inspekta Mwala amekuwa wa hivi karibuni kulalamika na kusema kwamba kwa upande wake bei ya kopo la msalani ikiguswa tu hivi basi ako radhi kubadilisha dini na kuingia Uislam mazima.

“Wakigusa tu bei ya tissue nabadilisha dini,” aliandika Mwala kwenye Facebook yake.

Ikumbukwe kuna dhana zinazosemekana kwamba Waislamu huwa hawatumii makopo ya msalani kujipanguza baada ya haja kubwa ashakum si matusi bali wao hutumia mqaji kama mbadala ya ‘tissue’

Mwala ameichukulia hii na kusema kwamba iwapo bei ya bidhaa hiyo ikiguswa kwa kuongezwa basi hatakuwa na budi kubadilisha dini ambapo atakubaliwa kuenda na maji chooni badala ya kopo la msalani.

Baadhi ya mashabiki wake walimtupia utani kwa kumuuliza kama atarudi tena katika dini ya Ukristo iwapo maji yataadimika kama petroli ilivyoadimika wakati hii nchini Kenya.

Wewe ni nini bei yake ikipandishwa tu hivi utachukua maamuzi ya kuwashangaza wanaokujua?