Nilipunguza ulevi baada ya kupata ujauzito wa kwanza- Avril

Muhtasari

•Avril amesema alipunguza tabia yake ya kunywa pombe baada ya kupata ujauzito wa mtoto wake wa pekee.

•Katika kipindi hicho Avril pia alipongeza uteuzi wa Martha Karua kuwa mgombea mwenza wa , Raila Odinga.

Msanii Avril
Image: AVRIL/INSTAGRAM

Mwanamuziki mashuhuri Judith Nyambura almaarufu Avril amekiri kuwa mtumizi wa kileo aina ya Vodka.

Avril hata hivyo ameweka wazi kuwa yeye si mnywaji wa Pombe mara kwa mara. Amesema alipunguza tabia yake ya kunywa pombe baada ya kupata ujauzito wa mtoto wake wa pekee.

"Mimi hupendelea Vodka. Hapo awali nilikuwa nakunywa Whisky lakini imekuwa kali kiasi kwangu sasa kwa sababu sijakuwa nikilewa sana hasa baada ya ujauzito wangu. Sikunywa pombe yoyote katika kipindi hicho. Kwa sasa sikunywi pombe sana," Avril alisema katika kipindi cha maswali na majibu kwenye Citizen Digital.

Mama huyo wa mtoto mmoja pia alisema anafurahia hatua yake kuwa mzazi hasa kila  anapomtazama mwanawe akikua.

"Ninajiona sana ndani yake. Kila siku huwa siku tofauti. Huwa anajifunza kitu kipya," Alisema.

Avril alifichua kuwa anakusudia kupata angalau mtoto mmoja ana wawili zaidi. Hata hivyo alisema hayupo tayari kupata mtoto mwingine hivi karibuni.

"Mtoto mwenye niko naye kwa sasa ananikimbiza. Gharama ya kulea mtoto ni kubwa kila mahali. Ningependa kupata wengine wawili ama watatu. Kifungua mimba wangu anaweza kupata ndugu wengine. Kwa sasa naamini biashara yangu ndiyo mtoto wa pili," Alisema.

Katika kipindi hicho Avril pia alipongeza uteuzi wa Martha Karua kuwa mgombea mwenza wa mpeperusha bendera ya Azimio la Umoja, Raila Odinga.

Alisema anafurahia uteuzi huo kwa kuwa ni wakati muhimu kwa nchi ya Kenya huku akimtakia mafanikio azma yake ya siasa.

"Kuweza kujiinua jinsi alivyojiinua ni jambo la kufurahisha. Niko na picha naye. Namtakia kila la kheri. Ni wakati muhimu katika historia," Alisema.