Marioo aapa kuweka dibwi nyumbani kufuatia machungu ya kuona mpenziwe akiogelea na Diamond

Muhtasari

•Marioo amesema anakusudia kuweka bwawa nyumbani kwa kuwa mpenzi wake anapenda sana kuogelea.

•Diamond na Mars walirekodiwa ndani ya maji wakiwa wamevalia mavazi ya kuogelea huku  wakionekana wenye furaha tele

Marioo na mpenzi wake Mimi Mars
Marioo na mpenzi wake Mimi Mars
Image: INSTAGRAM// MARIOO

Staa wa Bongo Marioo ameahidi mpenzi wake Mimi Mars kuwa atahakikisha kwamba wanapata bwawa la kuogelea nyumbani kwao.

Marioo amesema anakusudia kuweka bwawa nyumbani kwa kuwa mpenzi wake anapenda sana kuogelea.

"Na nyumbani naweka swimming pool. Si unapenda kuogelea!!?" Marioo alimwambia mpenzi wake kupitia Instagram.

Mwanamuziki huyo aliambatanisha ujumbe wake na picha yake akikumbatia kipenzi hicho chake Mimi Mars.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya mtunzi huyo wa "Mi Amor" kufichua kuwa aliumia sana moyoni baada ya kuona video ya Bi Mars akijivinjari na Diamond ndani ya bwawa lake la kuogelea.

Tukio hilo lilitokea mwaka wa 2020 ambapo Diamond na Mars walirekodiwa ndani ya maji wakiwa wamevalia mavazi ya kuogelea huku  wakionekana wenye furaha tele.

Marioo akishirikisha mashabiki wake kwenye kipindi cha maswali na majibu kwenye Instagram alifichua kuwa hilo ndilo tukio ambalo limewahi kuumiza zaidi maishani.

"Yapo mengi ila nilivoonaga ile klipu video ya rafiki yangu wa kike anaogelea kwenye pool la broo ilinigusa nayo ile," Marioo alimjibu shabiki aliyeuliza kuhusu tukio ambalo limewahi kumuumiza zaidi.

Takriban miaka miwili iliyopita uvumi ulitanda kuwa Diamond na Mars wanachumbiana baada ya bosi huyo wa Wasafi kupakia video iliyonyesha Mars akinengua kiuno kwa wimbo wake  'Cheche.'

"Mi nakapendaga haka katoto…. Sema sjui ata Tyming naikoseaga wapi Mwana wa Dangote… Doh! @mimi_mvrs11 ….. #CHECHE,” Diamond aliandika chini ya video hiyo.

Baadae hata hivyo Mars alijitokeza kupuuzilia mbali madai kuwa yupo kwenye mahusiano na bosi huyo wa Wasafi.

Licha ya yaliyotokea awali ni wazi kuwa Marioo hana kinyongo chochote na Diamond kwa kuwa hata wanapanga kushirikishana kwenye wimbo.

Mpenzi wa Marioo, Mimi Mars ni dada mdogo wa malkia wa muziki wa Bongo Vanessa Mdee.