Diamond ajawa na wasiwasi baada ya mama yake kulazwa hospitalini

Muhtasari

•Diamond alipakia video inayomuonyesha mamake katika chumba cha hospitalini huku akiwa na sindano mkononi.

• Zuchu, wanafamilia na marafiki wa karibu ni miongoni mwa watu  ambao walimtembelea Mama Dangote.

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Mama ya Diamond Platnumz, Bi Sandra Kassim almaarufu Mama Dangote anaendelea kupokea matibabu baada ya kushambuliwa na maradhi.

Diamond  ambaye anaripotiwa kuwa nje ya Tanzania aliwafahamisha wafuasi wake kuhusu hali ya mamake Jumapili kupitia Instastori zake.

Mwanamuziki huyo alipakia video inayomuonyesha mamake katika chumba cha hospitalini huku akiwa na sindano mkononi. Aliambatanisha video hiyo na emoji inayoashiria mtu aliye na wasiwasi.

Msanii wake Zuchu, wanafamilia na marafiki wa karibu ni miongoni mwa watu  ambao walimtembelea Mama Dangote.

Dadake Diamond, Esma Platnumz pia alipakia video ya mama yao akiwa hospitalini na kutoa taarifa fupi kuhusu hali yake.

"Mgonjwa💉🩸," Esma aliandika chini ya video iliyoonyesha Mama Dangote akiwa katika chumba cha wagonjwa.

Hali yake hata hivyo sio ya kutia wasiwasi mwingi kwani licha ya kuwa yupo hospitalini alionekana mchangamfu.

Mama Dangote alionekana akizungumza vizuri na wote waliomtembelea na hata kujipatia chakula mwenyewe bila usaidizi wowote.

Haya yalijiri muda mfupi tu baada ya Diamond kuachia video ya wimbo wake na Mbosso 'OKA' ambao upo kwenye albamu ya FOA.