Ndoa na Zuchu? Diamond adokeza kufunga pingu za maisha hivi karibuni

Diamond hata hivyo alieleza hofu yake kuwa ndoa huenda ikazorotesha taaluma yake ya muziki.

Muhtasari

•Diamond Platnumz hata hivyo hajathibitisha tarehe halisi ambayo anakusudia kufunga pingu za maisha.

•Bosi huyo wa WCB hata hivyo alieleza hofu yake kuwa ndoa huenda ikazorotesha taaluma yake ya muziki.

Diamond na msanii wake Zuchu ambaye anadaiwa kuwa kwenye mahusiano naye
Diamond na msanii wake Zuchu ambaye anadaiwa kuwa kwenye mahusiano naye
Image: KWA HISANI

Diamond Platnumz amedokeza kutulia kwenye ndoa hivi karibuni.

Staa huyo wa Bongo hata hivyo hajathibitisha tarehe halisi ambayo anakusudia kufunga pingu za maisha.

"Wakati wowote hivi karibuni. Hatuwezi kujuua. Ni Mungu hupanga yote, sisi hutamani tu kama binadamu lakini Mungu ndiye hupanga kila kitu," Diamond alisema katika mahojiano na DW Afrika.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 32 alikuwa anajibu swali kuhusu wakati ambapo anapanga kutulia kwenye ndoa.

Diamond pia alitakiwa kuweka wazi ikiwa kwa kweli yupo kwenye mahusiano na Zuchu, swali ambalo aliliepuka.

"Ningetamani hata iwe kesho. Huwezi kujua kama nitafunga ndoa ama haitafanyika," Alisema.

Bosi huyo wa WCB hata hivyo alieleza hofu yake kuwa ndoa huenda ikazorotesha taaluma yake ya muziki.

Diamond hajakuwa kwenye mahusiano au ndoa yoyote  inayojulikana wazi tangu mwaka wa 2020.

Hata hivyo, katika miezi ya hivi majuzi amekuwa akionyesha wazi kwamba kuna mwanadada ambaye ameuteka moyo wake.

"Niko kwenye mahusiano. Nina furaha. Nafurahia, mahusiano yangu yananipa raha na amani. Huba limetaradadi, mahaba ndi ndi ndi" Diamond alisema mwezi Februari.

Kwa muda mrefu mwaka huu staa huyo amekuwa akidaiwa kuwa kwenye mahusiano na msanii wake Zuchu.

Mapema mwezi huu Diamond alijitambulisha hadharani kama mume wa malkia huyo kutoka Zanzibar kwa mara ya kwanza.

"Huyo ni mume wa Zuuh," Alijibu chini ya video iliyomuonyesha akitumbuiza mashabiki wake nchini Ureno.

Siku chache baadae hata hivyo Zuchu alikana kuwa yeye ndiye aliyekuwa anazungumziwa na bosi huyo wake.

"Zuuh wako wengi. Ni kweli naitwa Zuuh lakini si Zuuh mimi, kama ingekuwa mimi angeniambia. Itakuwa Zuuh mwingine," Zuchu alijibu katika mazungumzo ya simu na mtangazaji wa Wasafi Media alipohojiwa kuhusu matamshi ya Diamond.

Katika mazungumzo hayo, Binti huyo wa Khadija Kopa bado alisistiza kuwa  uhusiano wake na Diamond ni wa kikazi.