Fahamu mara kadhaa ambayo Diamond Platnumz amedokeza yupo tayari kwa ndoa nyingine

Muhtasari

• Diamond alitangaza kuna malkia mpya kwenye ufalme wake na kuweka wazi kuwa anayathamini sana mahusiano yake mapya.

•Siku za hivi majuzi mamake Diamond amekuwa akimshinikiza apige hatua ya kumvisha pete mpenzi wake mpya ifikapo mwisho wa Ramadhan. 

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Katika kipindi cha miezi kadhaa ambacho kimepita, staa wa Bongo Diamond Platnumz amekuwa akionyesha wazi kwamba yupo kwenye mahusiano.

Mwezi Februari, Diamond alitangaza kuna malkia mpya kwenye ufalme wake na kuweka wazi kuwa anayathamini sana mahusiano yake mapya.

"Niko kwenye mahusiano. Nina furaha. Nafurahia, mahusiano yangu yananipa raha na amani. Huba limetaradadi, mahaba ndi ndi ndi" Diamond alisema.

Diamond alibainisha kuwa anampenda sana mpenzi wake huyo ambaye hakutambulisha.

"Nampenda sana. Yeye anafahamu nampenda. Maneno tupu hayatoshi, ila matendo yangu anayaona" Diamond alisema.

Baba huyo wa watoto wanne wanaojulikana alianza kudokeza kuwa tayari amezama katika bahari la mahaba takriban miezi mitatu iliyopita. Hii ilikuwa baada yake kupokea zawadi la viatu vya thamani kutoka kwa aliyetambulisha kama "Baby" (Mpenzi)

"Hii Bottega original. Nimeletewa na mke wangu. Baby kaniletea kutoka sehemu tu. Hazitoka Tanzania, nje. Ni zawadi kutoka kwa mpenzi wangu. Bottega halisi!" Diamond alisema alipokuwa anarekodi video ya wimbo wake 'Unachezaje'

Diamond hata hivyo alikataa kutambulisha jina la mpenzi huyo wake huku akidai hata jina lake halipatikani hata kwa Google.

"Mimi singenunua, najijua. Kiatu ni ghali... hutapata kwa Google, hayuko pale" Diamond alisema.

Takriban miezi miwili iliyopita dunia ilipokuwa inaadhimisha msimu wa wapendao, tetesi ziliibuka kwamba mwanamuziki huyo alikuwa anapanga ndoa na msanii wake Zuchu.

Wengi waliamini kuwa malkia huyo wa muziki kutoka Zanzibar ndiye aliyeteka moyo wa Simba. Hata hivyo, wawili hao walijitokeza kupuuzilia mbali madai hayo.

"Mimi sikai kwa Diamond. Kwa kweli nachumbiana na mtu, niko na boyfriend. Ni mtu tu wa kawaida. Ni mrefu kuliko mimi, ni maji ya kunde, ni mfanyibiashara na anafanya mazoezi. Siwezi kuwa na mtu ambaye hafanyi mazoezi, afya ni kila kitu" Zuchu alisema akiwa kwenye mahojiano na Wasafi Media.

Licha ya wanamuziki hao wawili kujitokeza kufafanua kuhusu uhusiano wao, madai kuwa wapo kwenye mahusiano bado yanaendelea kusikika. Ukaribu wao na muungano mzuri umeendelea kuibua maswali mengi na kuweka dhana ya mapenzi kwenye akili ya mashabiki wao wengi.

Siku za hivi majuzi mamake Diamond amekuwa akimshinikiza apige hatua ya kumvisha pete mpenzi wake mpya ifikapo mwisho wa Ramadhan.

"Nashindwa kuelezea furaha yangu mwanangu, Naseeb Diamond Platnumz🦁, hapa sasa umepata mwenza. Utulie babangu uoe.."  Mama Dangote alimwambia mwanamwe Diamond mapema wiki hii kupitia Instagram.

Huku mwezi mtukufu wa Ramadhan uking'oa nanga siku kadhaa zilizopita, Diamond alipokea msala miongoni mwa zawadi zingine kochokocho kutoka kwa mpenzi wake.

Diamond alionekana kuridhishwa sana moyoni na jambo hilo huku akimsifia mchumba huyo wake kwa makubwa aliyomfanyia.

"Kumpata anayekupenda ni jambo moja, ila kumpata atakayekuelewa na kukupa unachotaka ni jambo lingine kabisa," Diamond alisema.

"Simba anakupenda sana.. Wewe ni wangu wa kwanza na wa mwisho," Alimwandikia malkia huyo.

Matukio haya yanaashiria kwamba ndoa nyingine ya bosi huyo wa Wasafi huenda ikashuhudiwa hivi karibuni.