Tiktoker aliyeugua vibaya baada ya kula buibui hatimaye azungumza baada ya kudaiwa kufariki

Aq9ine amedokeza kuwa tayari amepata nyoka ambaye anakusudia kupika na kula hivi karibuni.

Muhtasari

•Aq9ine amepuuzilia mbali uvumi kuwa amefariki na kuwataka wanamitandao kutoamini chochote wanachokiona kwenye mitandao ya kijamii.

•Jumamosi aliripotiwa kukimbizwa hospitalini na kulazwa baada ya kifua chake kuanza kuuma na homa kali kumshambulia.

Image: INSTAGRAM// AQ9INE

Mtumbuizaji mmarufu wa Tiktok Aq9ine amejitokeza kuuzima uvumi kuwa alifariki baada ya kupika na kula buibui.

Siku ya Jumamosi, mtumbuizaji huyo alizua wasiwasi mkubwa miongoni mwa wanamtandao baada ya kupakia video iliyoonyesha jinsi sura yake ilivyoathiriwa vibaya baada ya kula mnyama huyo.

"Ikiwa hii ndio video yangu ya mwisho, imekuwa jambo la kufurahisha kuwaburudisha na kuhatarisha maisha yangu pia. Ninapenda hatari sababu tunaishi hatari. Sisi sote tutakufa. Nawapenda sana ndugu zangu," Aq9ine aliandika chini ya video hiyo ambayo alipakia kwenye Instagram.

Katika video hiyo Aq9ine ambaye alionekana kuwa na maumivu makali alionyesha jinsi uso na mikono yake ilivyokuwa imevimba.

Baadae anaripotiwa kukimbizwa hospitali na kulazwa baada ya kifua chake kuanza kuuma na homa kali kumshambulia.

"Aq9ine amelazwa baada ya kifua chake kuanza kuuma na homa ilikuwa nyuzi joto 48. Nitakaa nikiwafahamisha yote," Ujumbe ambao ulipakiwa kwenye Instastori zake baadae Jumamosi ulisoma.

Mtumbuizaji huyo sasa  ameonyesha picha mpya ya uso wake ambao tayari umepona kwa kiasi kikubwa.

Amewataka mashabiki wake kuishiwa na hofu huku akiwahakikishia kuwa sasa yupo buheri wa afya. Pia amedokeza kuwa tayari amepata nyoka ambaye anakusudia kupika na kula hivi karibuni.

"Ndio kufufuka.. Nimerudi na ile nyoka ya Garden of Eden. Si mnaona niko fiti. Msiwe na stress," Aliandika chini ya picha mpya aliyopakia kwenye ukurasa wake Jumapili.

Aq9ine pia alipuuzilia mbali uvumi kuwa amefariki na kuwataka wanamitandao kutoamini chochote wanachokiona kwenye mitandao ya kijamii.

"Alafu stori ni mob. Zingine ata si mimi, fake accounts nazo zimejaa. Kwanza naskia Tiktok mshanifanyia mazishi ati nimededi. Ahh wacha nicheke tu. Juu kufa nayo si jina iko kwa dictionary yangu. Msiamini kila mnachoona kwenye mitrandao ya kijamii," Aliandika Aq9ine.

Jumamosi mtumbuizaji huyo anayejulikana kwa kudhubutu kula wanyama tofauti alikumbana na ukosoaji mkubwa kufuatia hatua yake ya kula buibui.

Wanamitandao wengi ambao walionekana kukerwa na jambo hilo walimshauri akome huku wengine wakionya kuhusu matokeo mabaya.