Natamani ndoa! Dadake Diamond akiri makosa aliyofanya katika ndoa yake ya miezi 3

Esma amesema kwamba ndoa ni hatua ya lazima kwa kila mwanamke duniani.

Muhtasari

•Esma amedai kuwa alikimbilia kuingia kwenye ndoa hiyo bila kwanza kumfahamu vyema aliyekuwa  mumewe.

•Ameweka wazi kuwa tayari amempata mchumba wa chaguo lake ambaye angependa kufunga ndoa naye.

katika picha ya maktaba
Mama Dangote, Diamond Platnumz, Esma Platnumz katika picha ya maktaba
Image: INSTAGRAM// ESMA PLATNUMZ

Mfanyibiashara mashuhuri Bongo, Esma Platnumz amefunguka kuhusu sababu zilizopelekea yeye kugura ndoa miezi mitatu baada ya harusi.

Mnamo Agosti 2020, dada huyo mkubwa wa Diamond Platnumz alifunga pingu za maisha na mfanyibiashara Maulid Msizwa. Ndoa hiyo hata hivyo haikudumu kwani miezi mitatu tu baadae wawili hao walitengana.

Esma amedai kuwa alikimbilia kuingia kwenye ndoa hiyo bila kwanza kumfahamu vyema aliyekuwa  mumewe.

"Nahisi labda nilikurupuka na wasiwasi. Nilikuwa na haraka. Sikujipa muda wa kufikiria ikiwa ninayeolewa naye ni sahihi kwangu. Kipindi kile kilikuwa cha Corona, kulikuwa na stress nini. Nahisi nilikurupuka," Esma alisema katika mahojiano na Wasafi Media.

Licha ya kuwa aligura ndoa yake na Bw Msizwa baada ya kipindi kifupi, Esma amekiri kuwa anatamani sana kuoelewa tena.

Mama huyo wa watoto wawili alisema kwamba anaamini ndoa ni hatua ya lazima kwa kila mwanamke duniani.

"Natamani ndoa kwa sababu mimi ni mwanamke pia nahitaji heshima yangu. Nahitaji niolewe...  Mwanamke yeyote ndoa ni lazima,sio sisi, kidini ndoa ni lazima," Alisema.

Esma alifichua kuwa kuna wanaume wengi ambao wamekuwa wakijaribu kumtongoza kwenye mitandao ya kijamii.

Hata hivyo aliweka wazi kuwa tayari amempata mchumba wa chaguo lake ambaye angependa kufunga ndoa naye.

"Mwanaume ambaye nahitaji ni yule ambaye niko naye sasa hivi. Ni mfanyibiashara,mwanaume ambaye anajielewa na ni mfanyikazi hasa. Tunajuana mimi naye na labda watu wa karibu," Alisema.

Mama huyo wa watoto wawili aliweka wazi kuwa kuvunjika kwa ndoa yake kulimfanya kuwa mwangalifu zaidi kwani hangetaka kurudia makosa ya awali.

"Watu ambao nakutana nao sasa hivi. Mimi ndio napangua. Najaribu kuingia, nikiona sielewi basi naachana naye. Nikiona ninachokihitaji kwako hakipo naona nimove on niendelee na maisha yangu," Alisema.

Kufikia sasa Esma amewahi kuwa kwenye mahusiano mengi ambayo hayakudumu. Ana watoto wawili kutoka kwa mahusiano yake ya awali.