"Mwanaume hawezi kunibabaisha!" Dadake Diamond aeleza kwa nini ndoa zake hazidumu

Ndoa ya kwanza ya Esma ilidumu kwa kipindi cha miezi mitatu tu.

Muhtasari

•Esma amekana madai kuwa shida  ya kukosa kutulia kwenye ndoa moja  kwa muda mrefu hutokana na ustaa unaomuingia kwa kuwa dadake Diamond.

•Aliweka wazi kwamba kamwe hajawahi kujinufaisha  kwa umaarufu wa kaka yake wala kutegemea mali yake.

Mjasiriamali Esma Khan, dada mkubwa msanii Diamond Platnumz
Mjasiriamali Esma Khan, dada mkubwa msanii Diamond Platnumz
Image: Instagram

Mfanyibiashara Esma Platnumz amepuuzilia mbali madai kuwa shida  yake ya kukosa kutulia kwenye ndoa moja  kwa muda mrefu hutokana na ustaa unayomuingia kwa kuwa dada mkubwa wa mwanamuziki Diamond Platnumz.

Esma amedai kwamba kamwe hajawahi kujipiga kifua kuhusu uhusiano wake na bosi huyo wa WCB.

"Sijawahi kusema eti kujigamba mimi ni dadake fulani. Nikiwa na mtu mwingine siwezi kusema eti mimi ni dadake fulani," Esma alisema katika mahojiano ya hivi majuzi na Wasafi Media.

Mama huyo wa watoto wawili alibainisha kuwa kwa kawaida huwa anamtaja kakake kwa jina lake rasmi wala sio jina la jukwaani.

Alieleza kwamba sababu kuu inayochangia kusambaratika kwa mahusiano yake ni ukosefu wa maelewano kati yake na mwenzie.

"Mimi sijimwambafai eti kwa sababu mimi ni dadake fulani. Mimi ninajiamini na ninajikubali kwa sababu mimi ni mwanamke anayetafuta mwenyewe. Najua kutafuta pesa , najua kujilipia kodi , najua kujijengea, najua kulisha watoto  wangu. Pia nina wafanyikazi nyumbani, ninasomesha watoto wangu kwa gharamu. Kwa hiyo mwanaume hawezi kunibabaisha , ndugu yangu nikiona hatuelewani basi shika huko nami nishike huku. Maisha mafupi na nishateswa huko sana," Alisema.

Aidha aliweka wazi kwamba kamwe hajawahi kujinufaisha  kwa umaarufu wa kaka yake wala kutegemea mali yake.

Licha ya kuhangaika sana katika mahusino yake ya awali, Esma alitangaza kwamba amepata ambaye anatazamia kufungua ndoa ya pili naye.

Alisema kuna mwanga kwenye mahusiano yake ya sasa na kumuomba mchumba wake kufanya mpango wa harusi.

"Huyu nazaa naye. Kwanza tushafanya mpango kabisa, mwaka huu hauishi tunapata mtoto wetu wa kiume, ata wa kike yeyote ambaye atakuja. Huyu tutadumu naye milele. Nampenda sana," Alisema.

Alisema anampenda mpenzi wake wa sasa kwa kuwa ni mtanashati na mwenye bidii ya kutafuta pesa.

Hii haitakuwa ndoa ya kwanza kwa Esma. Julai 2020 mfanyibiashara huyo aliolewa na Bw Msizwa kama mke wa tatu ila wakatengana hata kabla ya mwaka huo kuisha. 

Ndoa ya kwanza ya Esma ilidumu kwa kipindi cha miezi mitatu tu.