"Baba nani!" Juliani hatimaye ajitokeza na mtoto wake na Lilian Nganga

Juliani ana mtoto mwingine na mpenzi wake wa zaman, muigizajii Brenda Wairimu.

Muhtasari

•Rapa huyo alionekana akiwa amesimama nje ya lango huku akiwa ameamshika kijigari cha kubebea mtoto.

•Mwimbaji huyo hata hivyo hakuonyesha sura ya mtoto huyo wake wa pili.

Juliani katika matembezi na mwanawe
Image: INSTAGRAM// JULIANI

Jumamosi, mwimbaji wa nyimbo za kufoka Julius Owino almaarufu Juliani kwa mara ya kwanza alipakia picha yake akiwa kwenye matembezi na mwanawe.

Katika picha ambayo alichapisha Instagram, rapa huyo alionekana akiwa amesimama nje ya lango huku akiwa ameamshika kijigari cha kubebea mtoto.

Chini ya picha hiyo Juliani alinukuu mstari wa Biblia kutoka kitabu cha Mwanzo 17:6.

"Nitakufanya uzae sana: nitafanya mataifa yako, na wafalme watatoka kwako," 

Mwimbaji huyo hata hivyo hakuonyesha sura ya mtoto huyo wake wa pili.

Image: INSTAGRAM// JULIANI

Mapema mwezi jana, Juliani alitangaza kuzaliwa kwa mtoto wake wa kwanza na aliyekuwa mwenzi wa gavana wa zamani wa Machakos, Lilian Nganga.

Katika mahojiano na Presenter Ali, rapa huyo alisema mkewe alijifungua mtoto wa kiume na kuelezea furaha yake kubwa kwa kuwa baba tena .

"Nina watoto wawili. Msichana na mvulana. Nilimkaribisha mtoto wa kiume hivi majuzi na Lilian Ng'ang'a," alisema kwa furaha na tabasamu.

Aliongeza, ""Sikutaka kusema mengi kuhusu hilo lakini tulipata mtoto kwa hiyo mimi ni baba wa watoto wawili. Ukweli ni kama baba kwa mtoto wa kiume, hauhusiki sana."

Ujauzito wa Bi Lilian ulikuja kufichuka mwezi Februari baada ya kuchapisha video iliyoonyesha tumbo lake likiwa limechoza.

Katika video hiyo mke huyo wa zamani wa Alfred Mutua alionekana akijivinjari ufukweni huku akionekana mwenye bashasha tele.

"Siku ya wapendanao 2022" Lilian aliandika chini ya video hiyo.

Lilian na Juliani walifunga pingu za maisha mapema mwaka huu katika hafla ndogo iliyofanyika katika kiwanja cha Paradise Garden ambayo ilihudhuriwa na familia na marafiki wachache wa karibu .

Wawili hao walijitosa kwenye mahusiano ya kimapenzi kipindi kifupi tu baada ya Lilian kutengana na Bw Mutua.

Juliani ana mtoto mwingine na mpenzi wake wa zamani Brenda  Wairimu. Wawili hao ambao walitengana 2018 walibarikiwa na mtoto wa kike takriban miaka nane iliyopita.