(+video) Mchungaji achukizwa na vijana wadogo kupendana na wazee "Unakula mali ya babu?"

Nenda tafuta size yako tunataka watoto - Mgogo

Muhtasari

• Vijana tunategemea waoe tufunge harusi, watuletee wajukuu - Mgogo.

Mchungaji maarufu kutoka Tanzania, Daniel Mgogo amelivalia njuga suala la vijana wadogo kuingia kweney mahusiano ya mapenzi na wazee waliowazidi umri mara dufu.

Akizungumza katika moja ya ibada zake za mitandaoni, mchungaji Mgogo amewazomea vijana hao na kuwataka kujiepusha na mitego kama hiyo kwani tabia hiyo ni kama kushiriki katika kula mali ya babu yako aliyetangulia mbele ya haki kitambo.

Mgogo pia hakuwasaza wakongwe hao wanaojiingiza katika mapenzi ya vijana wadogo, wake kwa waume akiwataka kujiheshimu na kukoma kuwapotosha vijana kwani kanisa linataka vijana wengi kufanya harusi na vijana wenzao ili kukuza kizazi kijacho.

Mgogo akionesha kuchukizwa, alipinga vikali dhana kwamba umri ni namba tu na kusema kwamab hakuna vile vijana wanaweza ingia katika mapenzi na wazee na mahusiano hayo kutarajia kupata watoto wa kuendeleza kizazi cha usoni.

“Kijana mbichi anajihusisha kimapenzi na jimama. Baba zake walijishughulisha naye ana hili baba zake walizaa watoto na huyu mama na wewe unaenda, utazaa watoto na huyu ana miaka sabini. Alafu mnatuambia, umri namba. Vijana tunategemea waoe tufunge harusi, watuletee wajukuu. Watu wanasukumana na mabibi minyanya,” Mchungaji Mgogo alitema moto.

Aliwakashfu vijana wengi siku hizi ambao wanatebwereka na kusubiria embe kudondoka kutoka mtini pasi na kufanya juhudi zozote za kukwea ili kulichuma lile embe kwa nguvu zao.

Kulingana na yeye, vijana hao wanafanya kula mali za babu zao jambo ambalo amechukizwa nalo.

“Kweli kijana mdogo jitegemea, unataka kula mali za babu yako aliyekufa alimuacha huyu bibi. Wachana na huyo mama! Nenda tafuta size yako tunataka watoto,” Mgogo alisisitiza.

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na matukio yasiyo ya kawaida ambapo unawapata vijana wadogo wanajihusisha katika mahusiano ya kimapenzi na ajuza na babu waliopitwa na umri na unapata baadhi ya watu wanashabikia mahusiano hayo, jambo ambalo kwa mchunaji Mgogo si kitu cha kufurahisha bali kukemewa vikali kwa sababu wengi wakilikumbatia basi kizazi cha kesho hakimo.