"Nitavunja hiyo miguu!" Zuchu amuonya mumewe dhidi ya kumletea mke mwenza

Staa huyo alimtaka mpenziwe kutulia na kuepuka kutoka nje ya mahusiano yao.

Muhtasari

•Kupitia mtandao wa kijamii, staa huyo amemuonya  mpenzi wake dhidi ya kuwahi kuwa na mke mwingine.

•Kwa muda mrefu sasa, Zuchu amekuwa akihusishwa kimapenzi na bosi huyo wake Diamond Platnumz.

ZUCHU NA DIAMOND PLATNUMZ
Image: WASAFI/INSTAGRAM

Malkia wa Bongo Zuhura Othman Soud almaarufu Zuchu ametoa onyo kali kwa mpenzi wake na kutoa tishio.

Kupitia mtandao wa kijamii, staa huyo amemuonya  mpenzi wake dhidi ya kuwahi kumletea mke mwenza.

Alitumia meme iliyomuonyesha Haji Manara akiwa pamoja na wake zake wawili kutoa onyo lake, ambapo alitishia kuvunja miguu ya mpenziwe iwapo atawahi kufuata nyayo za msemaji huyo wa Yanga FC

"Jamani mume wangu, usijaribu huu mchezo!! Nitavunja miguu!" yalisomeka maelezo ya meme hiyo.

Binti huyo wa gwiji wa taarab ,Khadija Kopa, alimtaka mpenziwe kutulia na kuepuka kutoka nje ya mahusiano yao.

"Mpendwa Bebi kaa kwa kutulia," aliandika chini ya meme hiyo.

Zuchu aliambatanisha chapisho lake na beti ya wimbo wake mpya wa 'Kwikwi' ambapo anamshauri mpenzi wake kutimiza ahadi alizotoa kwa za kumlinda yeye pamoja na mahusiano yao daima.

Image: SNAPCHAT// ZUCHU

Haya yanajiri hata kabla mashabiki wake hawajaweza kutatua kitendawili cha iwapo anachumbiana  na Diamond Platnumz. Kwa muda mrefu sasa, Zuchu amekuwa akihusishwa kimapenzi na bosi huyo wake.

Siku chache zilizopita, Diamond kwa mara nyingine aliweka wazi kuwa uhusiano wake na Zuchu ni wa kikazi tu. Diamond alikana wazi uhusiano wa kimapenzi na mtunzi huyo wa kibao 'Sukari' na kusisitiza kuwa ni msanii wake tu.

Bosi huyo wa WCB alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya mmoja wa mameneja wake , Hamisi Shaban Taletale almaarufu Babu Tale, kumpa shinikizo kubwa  la kumuoa binti huyo wa gwiji wa muziki wa taarab ,Khadija Kopa.

"Fanya basi uoe unanichelewesha ujue," Tale alimwambia bosi huyo wa WCB chini ya video aliyopakia kwenye Instagram ikimuonyesha Zuchu akimkabidhi mkufu ghali wa dhahabu kama zawadi ya siku ya kuzaliwa.

Diamond ambaye alionekana kutofurahishwa na ujumbe huo wa meneja wake alihoji jinsi angeweza kumuoa msanii wake.

"Sasa nitamuoaje wakati ni msanii wangu Boss?" alihoji. 

Katika jibu lake, pia alifafanua kuhusu busu  aliloonekana akimpa Zuchu kwenye video hiyo ambayo amefuta tayari.

"Hilo busu hapo lisiwatishe viongozi.. ni Salaam za Kijerumani hizo," alisema.