(+video) Mvulana alia kwa hisia katika harusi ya dadake, hataki aolewe

Mvulana huyo mwenye umri wa baleghe alionekana kujawa na hisia na kuachia kilio huku watu wakimfariji.

Muhtasari

• Anaonekana akilia kwikwi bila kujizuia huku akielekeza macho yake upande mwingine kwani ulikuwa ni uchungu kumuona dadake kwa mara ya mwisho.

Ndoa ni Baraka na ni ndoto ya kila mtu mwenye akili razini. Huku familia ya mume inapofurahia kumpokea mtu mpya kwenye familia yao, kwa upande wa kina msichana huwa ni hisia mseto, wengi hujawa na machozi ya kumuaga mwenzao ambaye sasa anavuka na kujiunga na familia ya kina mume, akiiacha familia aliyokulia!

Ndivyo matukio yalivyokuwa katika harusi moja iliyorekodiwa na klipu kupakiwa kwenye mitandao ya kijamii.

Katika video hiyo ambayo sasa imesambazwa mno, mvulana mmoja anaonekana akidhibitisha upendo wa dhati kwa dadake ambaye ni bi harusi.

Mvulana huyo alitokwa na machozi siku ya harusi ya dada yake alipokaribia kuhama na kuishi na mumewe. Anaonekana akilia kwikwi bila kujizuia huku akielekeza macho yake upande mwingine kwani ulikuwa ni uchungu kumuona dadake kwa mara ya mwisho na kumpa kwaheri anapojiandaa kujiunga na familia ya kina bwana harusi.

Ishara ya kulia kwa kijana huyo ilivutia hisia na maoni kinzani kutoka kwa wanamitandao ambao wengine walitumia fursa hiyo kuzua utani.

“Huyo Analia kwa sababu anajua sasa kazi zote za ndani kama kufagia, kupika na kuosha vyombo itakuwa yake,” mmoja kwa jina Kevin alizisoma akili za yule kijana kwa utani.

“Bado ni mdogo, analia juu ya wajibu, au kuzama kwa upendo na mwanamke mwingine, akitaka kumuoa,” Hassan Hatam alisema.

“Ni kama kaka yangu lakini nilimwambia kaka unalia kwa sababu nimeolewa au una wasiwasi sitakuunga mkono baada ya harusi yangu,” Ngina Mushi alisema.

Wengine walijiweka katika viatu vya kijana huyo na kusema kwamba ni rahisi machozi kumtoka mtu haswa anapomuaga ndugu yake ambaye wamekuwa pamoja tangu utotoni na kujua kwamba hatoenda kuishi pamoja naye tena bali ataenda kuwajibika kwingine.

“Ndicho kilichotokea wakati wa ndoa ya dada yangu mzee wetu hakuweza kuacha kulia. Mungu aibariki ndoa yako,” Rita Hodur alikumbuka.