Masaibu yakumba ndoa ya Hamisa Mobetto baada ya kukiri mahaba mazito Mbappe

Mobetto alidokeza anavutiwa na Mbappe na kudai anajifunza Kifansa kwaajili yake.

Muhtasari

•Mobetto kukiri mahaba mazito kwa mshambuliaji matata wa Ufaransa Kylian Mbappe huenda kumeibua matatizo katika ndoa yake.

•Katika maelezo ya meme hiyo, Mobetto aliweka wazi kuwa hali sawa na iliyompata mwanadada huyo imemkuta pia.

Kylian Mbappe na Hamisa Mobetto
Image: INSTAGRAM

Hatua ya Hamisa Mobetto kukiri mahaba mazito kwa mshambuliaji matata wa Ufaransa Kylian Mbappe huenda imeibua matatizo katika ndoa yake, mwanamitindo na mwimbaji huyo wa Tanzania sasa amefichua.

Siku ya Jumatatu, mama huyo wa watoto wawili alidokeza kuwa anavutiwa na Mbappe na kudai kwamba anajifunza Kifansa kwaajili yake.

"À se damner🥰 (Nakukufia)," aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

"Najifunza kifaransa kwaajili ya #mbappe," alieleza.

Mpenzi huyo wa zamani wa staa wa Bongo Diamond Platnumz na ambaye ni mzazi mwenza wake aliambatanisha ujumbe huo na picha yake nzuri inayoonyesha akiwa ameshika tumbo lake huku akionekana mwenye mawazo. 

Baadae siku ya Jumanne, mwanamitindo huyo alichapisha meme kueleza hali iliyopata ndoa yake baada ya kukiri kumpenda Mbappe.

"Mume wangu kipenzi nywele zimefumuka kesho nataka kwenda kusuka naomba hela," mwanadada mmoja alimwandikia mumewe kwenye mtandao wa WhatsApp katika meme ambayo Mobetto alichapisha.

"Kamuombe Mbappe😑," Mumewe alijibu.

Katika maelezo ya meme hiyo, Mobetto aliweka wazi kuwa hali sawa na iliyompata mwanadada huyo imemkuta pia.

"Hali yangu kwa sasa🤣🤣🤣 Yamenikuta," aliandika.

Mobetto ni miongoni tu mwa wanadada wengi ambao wametekwa moyo na mshambuliaji huyo wa PSG hasa baada ya mchezo wake mzuri katika fainali ya Kombe la Dunia ambayo ilifanyika siku ya Jumapili ugani Lusail, nchini Qatar.

Mapema mwaka huu, Hamisa Mobetto alitangaza wazi kwamba amezama kabisa kwenye dimbwi la mahaba.

Katika video aliyochapisha mitandaoni, mzazi mwenza huyo wa staa wa Bongo Diamond Platnumz alikiri mapenzi yake mazito kwa mpenzi wake mpya na kufichua kuwa yuko tayari kufunga ndoa naye.

"Hatimaye nimepata mtu. Nimepata mwanaume ambaye nahisi ni yeye nataka. Nahisi kama kwamba huyu ndiye mtu ningependa kushiriki maisha yangu yote naye," alisema kwa kujivunia na msisimko mkubwa.

Mobetto aligamba kwamba hatimaye amefanikiwa kupata mwanamume anayezungumza lugha ya mapenzi sawa na yeye.

"Kila kitu ni rahisi sana, kila kitu ni sawa" alisema.

Aidha alisema kuwa anatamani sana kuvishwa pete na mpenzi wake mpya na kuchukua majukumu ya mke.

"Nataka kuolewa naye. Nataka kuolewa na mtu wangu. Nataka kumpikia, nimuandalie nguo ili aende kazini. Je, hii ni ndoto? niamke? Ikiwa ni ndoto mtu tafadhali anichune niamke," alisema Mobetto.

Ingawa hakumtambulisha mpenziwe, Mobetto alimsifia sana na kusema kuwa yeye ndiye mume kamili kwake.